Dar es Salaam. Ni maumivu unapompoteza mpendwa wako uliyehangaika naye hospitali ukiwa na matumaini kwamba atakuwa na afya njema, lakini kwa bahati mbaya akafariki dunia.
Katikati ya majonzi hayo, unakutana na bili kubwa ya matibabu ya mgonjwa wako, ndugu mkielezwa kwamba mwili wake hauwezi kuondolewa chumba cha kuhifadhi maiti kutokana na kutokamilishwa kwa gharama za matibabu.
Taarifa hiyo hukoleza majonzi kwa familia kwa kuwa tayari fedha nyingi zimetumika kwenye matibabu, na fedha hizo zilipatikana kwa kuuza vitu mbalimbali kama samani za ndani, mifugo au vifaa vya kielektroniki.
Hospitali inazuia mwili wa marehemu ili kushinikiza familia yake itafute fedha za kulipa deni hilo, ndipo wachukue mwili wa mpendwa wao, jambo ambalo limekuwa likitazamwa vibaya na wanajamii kwamba siyo uungwana.
Jambo hilo limekuwa likiumiza familia nyingi, hasa zisizo na uwezo, kwani wanashindwa kuwazika wapendwa wao kwa staha kutokana na ukosefu wa fedha. Kutokana na malalamiko hayo, Serikali imeamua kuingilia kati jambo hili.
Katika uzinduzi wa kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) za uchaguzi mkuu Agosti 28, 2025, Mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia alikuwa mgombea urais, Samia Suluhu Hassan, pamoja na mambo mengine, aliahidi kwamba ndani ya siku 100 za kwanza baada ya kuchaguliwa, watapiga marufuku hospitali yoyote nchini kuzuia miili ya marehemu kuchukuliwa na ndugu zao, hata kama gharama za matibabu aliyopatiwa ndugu yao hazijalipwa.
Alisisitiza watakuja na mfumo mwingine wa kuhakikisha jamaa wa marehemu wanalipa, lakini siyo kuzuia miili ya watu waliotangulia mbele za haki.
Kutokana na malalamiko ya wananchi ya muda mrefu kuhusu kuzuiliwa kwa miili ya ndugu zao, Desemba 25, 2020, aliyekuwa Waziri wa Afya, Dk Doroth Gwajima, akizungumza na madaktari na viongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila, aliagiza hospitali zote nchini kuweka utaratibu wa kufuatilia namna mgonjwa anaweza kulipia gharama za matibabu akiwa hai na sio kusubiri afariki dunia kisha wazuie maiti.
Mbali na tamko hilo, suala hilo liliendelea kutokea hata baada ya Serikali kutoa Waraka Namba Moja wa mwaka 2021 wa kutozuia maiti na kuweka utaratibu wa kulipa gharama za matibabu na madeni kwa wagonjwa waliofariki dunia.
Pamoja na kuwepo kwa mwongozo huo, malalamiko ya wananchi juu ya miili ya ndugu zao kuendelea kuzuiliwa yaliendelea kusikika, na aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alipiga marufuku tabia hiyo.
Ummy alitoa marufuku hiyo akiwa katika ziara ya aliyekuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda, Januari 20, 2024, mkoani Tanga, kuliibuka malalamiko ya wananchi juu ya tabia hiyo.
Desemba 8, 2025, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, aliagiza hospitali zote nchini kuanza mara moja utekelezaji wa katazo la kuzuia maiti, akisisitiza agizo hilo ni la lazima na halitakiwi kukaidiwa.
Mchengerwa alitoa ahadi hiyo wakati akizungumza kwenye kikao kazi na watumishi wa sekta ya afya jijini Dar es Salaam.
Katika kutekeleza agizo hilo ndani ya siku 100 za Rais Samia, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge, amesema msamaha uliotolewa kwa watu waliofariki dunia hadi sasa ni sita, kutokana na gharama za matibabu walizokuwa wakidaiwa, jumla ya Sh22.05 milioni, na kuruhusu miili kuchukuliwa na ndugu zao.
“Wagonjwa waliopatiwa msamaha wa fedha za matibabu kuanzia Novemba – Januari 22, 2026 ni 122, watu wazima wakiwa 52 na watoto 70. Fedha ambazo Serikali imechangia kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa hao ni Sh698.4 milioni. Wagonjwa waliopata msamaha wa huduma zinazotolewa katika kliniki ya moyo (Consultation) walikuwa 177, ambapo kati yao wanawake ni 76 na wanaume ni 101. Gharama ambazo Serikali imechangia kwa wagonjwa hao kupata huduma za kliniki zilikuwa Sh2.7 milioni,” amesema Dk Kisenge.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dk Jonas Lulandala, amesema ndani ya siku 100 za Rais Samia, suala la kuzuia maiti halipo, kwa kuwa tayari walikuwa na utaratibu mzuri wa kutoa huduma.
“Tumeweka utaratibu wa kuhakikisha hakuna mwili hata mmoja utakaozuiwa, jambo hili ni endelevu. Pia, katika siku hizi 100, tuna kiwango cha kutosha cha dawa,” amesema.
Mbali na hatua hiyo, Dk Lulandala amesema wameendelea kuimarisha utoaji wa huduma pamoja na vipimo vyote vinavyofanyika, ikiwemo kipimo cha homa ya ini (Hepatitis) aina B, na hospitali hiyo ni miongoni mwa hospitali chache zinazotoa huduma hiyo.
Pia, amesema hospitali hiyo imepokea watumishi mbalimbali watakaokwenda kusaidia maboresho ya huduma kuelekea Huduma ya Bima ya Afya kwa Wote, ambapo tayari Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeanza kusajili wanufaika.
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mount Meru, Dk Alex Ernest, amesema katika kutekeleza ahadi ya Rais Samia, hospitali hiyo imeweka utaratibu ambapo miili ya ndugu walioshindwa kulipia inatolewa mara moja.
Amesema utaratibu waliouweka ndugu hupewa mwili bila kikwazo, na kama kuna taratibu za malipo haziwezi kuathiri ndugu kuchukua mwili wa ndugu yao.
“Kwa sasa, Hospitali ya Mount Meru, ndugu wanaposhindwa kulipia huduma hupewa mwili, na kama taratibu za malipo zitafuata baadaye.
“Tangu tumeanza utaratibu huu ndani ya siku 100, zaidi ya Sh16.45 milioni zimesamehewa kwa ndugu wa wagonjwa waliofariki na kufika dawati letu kuomba mwili ili wahifadhi,” amesema.
Pia amesema utaratibu wa kuwahudumia wagonjwa wenye magonjwa sugu, kama alivyoahidi Rais Samia, umekuwa ukiwawezesha wananchi kupata huduma bila kikwazo.
Akizungumza kuhusu siku 100 za Rais Samia, Samson Jumbe, mkazi wa Kinyerezi, jijini Dar es Salaam, amesema kwa siku 100 za kwanza za kiongozi huyo madarakani, ameonesha mabadiliko ya mtazamo wa uongozi na kuleta matumaini mapya kwa wananchi.
Ameeleza hatua za awali zimekuwa za kusikiliza maoni ya wananchi na kupunguza hofu ya kisiasa, akisisitiza kuwa suala la wananchi kupunguzia mzigo wanapofiwa na ndugu zao ni jambo kubwa.
“Siku 100 za kwanza zimeonesha dhamira ya kurejesha imani kati ya Serikali na wananchi,” amesema. Kuhusu suala la kuzuia maiti mochwari, Joachim Pedro amesema uamuzi huo umeibua maswali mengi ya kisheria na kimaadili katika jamii.
“Kuzuia maiti kwa sababu ya fedha si sawa, ni muhimu maelekezo haya yametolewa kwa sababu ndugu walikuwa wanapata msiba juu ya msiba,” amesema.
Waraka namba moja wa mwaka 2021 wa kutozuia maiti na kuweka utaratibu wa kulipia gharama za matibabu na madeni kwa miili unaeleza utaratibu wa kuchukua mwili wa marehemu katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Sehemu ya 3.1.2 inaeleza iwapo marehemu alikuwa anahudumiwa kwa msamaha wa matibabu, ndugu waruhusiwe kuchukua mwili wa marehemu. Vilevile, sehemu ya 3.1.3 waraka huo unasema: “Iwapo marehemu alikuwa anachangia gharama za matibabu na mauti yamemfika akiwa na deni la gharama za matibabu, ndugu aruhusiwe kuchukua mwili baada ya kufanya malipo.”
Msisitizo umewekwa pia, sehemu ya 3.1.4 ya waraka huo kwamba iwapo ndugu wa marehemu hawatakuwa na uwezo wa kulipa deni pale mgonjwa atakapokuwa amefariki, ndugu wataingia makubaliano ya maandishi na kituo cha kutolea huduma ya namna ya kulipa deni, na waruhusiwe kuchukua mwili.