UWT Shinyanga yasitiri wasichana kwa taulo za hedhi

Shinyanga. Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga umetoa taulo za hedhi kwa wasichana wenye uhitaji katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 49 ya chama hicho.

Akizungumza leo Februari 09, 2026 Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Shinyanga Mjini, Rehema Nhamanilo amewataka wanafunzi wa shule hiyo, kujiepusha na vishawishi vya wanaume na badala yake wajikite katika masomo ili kutimiza ndoto zao.

“Tumekuja kuzungumza nanyi kama wazazi wenu, tunawasihi msome kwa bidii, msikubali kudanganywa kwa chipsi au kushawishiwa na wanaume ambao hawawatakii mema, kataeni na semeni tunasonga mbele, taulo hizi zitawasaidia kusoma bila changamoto wakati wa hedhi,” amesema Nhamanilo.

Naye, Kaimu Mkuu wa hiyo,  Simon Lange ameishukuru UWT kwa zawadi za taulo za kike, akisema zitasaidia wanafunzi wenye uhitaji kujisitiri wakati wa hedhi.

Lange ameongeza kuwa,  “Shule ilianzishwa Agosti 13, 2023 ikiwa na wanafunzi 73 na hadi kufikia mwaka 2026 ina wanafunzi 859, tukiwa na mafanikio makubwa kielimu katika Manispaa ya Shinyanga.”

Kwa niaba ya wanafunzi, Astelia Kimese, ameishukuru UWT Wilaya ya Shinyanga kwa kuwakumbuka na kuwapatia taulo za kike, akisema zitawasaidia wasichana wenye uhitaji kuendelea na masomo bila changamoto wakati wa hedhi.