DROO ya mechi za hatua ya 64-Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) imefanyika jana na vigogo va Ligi Kuu Bara ikiwamo, Simba, Yanga, Azam FC na Singida Black Stars zikipangwa na timu zinazoonekana mchekea katika hatua hiyo kusaka tiketi ya kusaka uwakilishi wa michuano ya CAF.
Katika droo hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Simba ambayo inalisotea taji la michuano hiyo kwa misimu minne mfululizo, imepangwa kuvaana na Greenland, ilihali watetezi wa taji hilo, Yanga watacheza na mabingwa wa zamani wa Ligi ya Bara msimu wa mwaka 1968, Cosmopolitan.
Kwa mujibu wa Meneja wa mashindano hayo yanayotoa mwakilishi wa nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika, Baraka Kizuguto amesema mechi za hatua hiyo zitapigwa kati ya Februari 17 hadi 19, lakini itategemeana na matumizi ya viwanja na washindi watafuzu hatua ya 32=Bora.
“Ratiba kamili ndiyo hiyo kutakuwa na siku tatu za michuano ya Kombe la Shirikisho, lakini itategemeana na matumizi ya viwanja wengine watawahi na wengine watachelewa kidogo,” amesema Kizuguto.
Kwa mujibu wa ratiba ya droo hiyo ya jana, Wanafainali wa 2022, Coastal Union wataikaribisha Nyumbu ya Pwani kwenye Uwanja wa Mkwakwani, wakati TZ Prisons itaumana na Moro Kids, huku Mbeya City itavaana na Biashara United na TRA United itamenyana na Rhino Rangers.
Mechi nyingine zinaonyesha kuwa maafande wa JKT Tanzania wataumana na Mabingwa wa Tanzania wa 1982 Pan Africans, huku mabingwa michuano hiyo kwa mwaka 2018 Mtibwa Sugar watavaana na IAA SC, huku Fountain Gate itamalizana na Mapinduzi.
Namungo yenyewe itavaana na Magnet FC, wakati Pamba Jiji itamalizana na ‘ndugu’ zao wa Mwanza, Alliance FC, ilihali Dodoma Jiji itapepetuana na Kilimanjaro Wonders, ambao msimu uliopita ilipasuliwa na Simba kwa mabao 6-0 katika hatua kama hiyo hii.
Kwa upande mwingine, mabingwa wa mwaka 2019, Azam FC wamepangwa na Endument FC kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, huku Singida Black Stars itacheza na Copco FC ya Mwnza na KMC FC itavaana ‘Mabaharia’ wa Bandari Tanzania.
Mechi nyingine zitakazopigwa ni vinara wa msimamo wa Ligi ya Championship, Geita Gold itaialika Kajuna FC, Kengold itacheza na Magereza, B19 FC dhidi ya Dhujau, huku Mbuni na The Green FC zitamalizana jijini Arusha, wakati Kagera Sugar itaumana na Mighty Elephants.
Pia Mbeya Kwanza itaumana na FGA Talents, Transit Camp dhidi ya Chama la Wana, Barberian itakwaruzana na Kijiwe Nongwa ilihali Songea United itacheza na Vijana FC na Gunners na Airport FC zitakwanyuana pia Bigman itakuwa na kibarua mbele ya Nyika FC.
Mechi nyingine ni kati ya TMA Stars v Newala FC, Polisi Tanzania v THB FC, Hausung FC v West Singers, Stand United v Mabao FC na mabingwa wa Ligi Kuu ya Muungano 1988 African Sports wataumana na Kilimo FC, jijini Tanga.
Michuano hiyo awali ilifahamika kama Kombe la FAT kabla ya kuwa Kombe la FA kuanzia 1967-2002 kisha kuzimika hadi liliporudi tena 2015-2016 likifahamika kama Kombe la Azam Sports (ASFC). Yanga ndio imelibeba mara nyingi ikiwa na tisa.