Dar es Salaam. Biashara katika Soko Kuu la Kariakoo zimeanza rasmi leo, huku changamoto mpya ikiibuka baada ya baadhi ya wachuuzi kuvamia vizimba vya wafanyabiashara wengine.
Soko hilo lilifunguliwa jana na Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa imetimia miaka mitano baada ya kuteketea kwa moto mwaka 2021 na kufanyiwa ukarabati mkubwa.
Licha ya wafanyabiashara wengi kuanza shughuli zao kwa furaha, baadhi ya waliokosa kupangiwa vizimba wamevamia maeneo ya wengine, hali iliyoibua malalamiko.
Mwananchi lilifika Kariakoo leo kufuatilia mwitikio wa wafanyabiashara, na mmoja wao aliyeomba asitajwe jina amesema aliingia kwenye kizimba kilichoonekana wazi kwa kuwa awali alikuwa akijitafutia riziki pembezoni mwa barabara.
Baadhi ya wananchi wakiwa wamejitokeza kufanya manunuzi katika Soko Kuu la Kariakoo leo Jumatatu, Februari 9, 2026.
Amesema yuko tayari kuondoka endapo mmiliki halali wa kizimba hicho atajitokeza, huku akiomba uongozi wa soko kuwazingatia wafanyabiashara wenye nia ya kufanya kazi katika soko hilo bila kuwawekea masharti magumu.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya viongozi wa wafanyabiashara wamethibitisha kuwepo kwa malalamiko hayo, wakisema wamepokea taarifa kutoka kwa wanachama wao kuwa walipokabidhiwa vizimba walikuta vimekaliwa.
Hata hivyo, Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko la Kariakoo, Ashraf Abdulkarim, amesema hajapokea malalamiko rasmi kuhusu suala hilo, akisisitiza uongozi wa soko utahakikisha ni wafanyabiashara waliokidhi utaratibu pekee ndio watakaoruhusiwa kufanya biashara ndani ya soko hilo.
“Si umeona pembezoni mwa vizimba, kuna namba maalumu, hiyo ndio kitambulisho cha mfanyabiashara aliyepata nafasi, ambacho anaweza kutuonesha katika nyaraka zake au hata kwenye simu kupitia mfumo maalumu alioombea ukaguzi utakaoanza muda wowote kuanzia sasa,” amesema na kuongeza kuwa hakutakuwa na janjajanja katika hilo.
Hata hivyo, upande wa wenye maduka hali imeonekana kuwa tofauti, kwani wafanyabiashara wengi bado hawajaanza shughuli zao, na hata waliofungua maduka hawakufiki kumi.
Baadhi ya wananchi wakiwa wamejitokeza kufanya manunuzi katika Soko Kuu la Kariakoo leo Jumatatu, Februari 9, 2026.
Mfanyakazi katika moja ya maduka, aliyeomba jina lake lisitajwe, amesema hali hiyo inatokana na ukweli kuwa biashara za dukani zinahitaji mtaji mkubwa ikilinganishwa na uuzaji wa mbogamboga na mazao mengine.
“Ili mfanyabiashara wa duka aweze kukaa kuna mpangilio atahitaji aufanye ili lionekane duka, lakini kwa mbogamboga na matunda hayo hata akiambiwa jioni aondoe vitu vyake aje navyo tena kesho asubuhi ni rahisi,” amesema mfanyakazi huyo.
Pia amesema mitaji ya biashara inatofautiana, ukizingatia wengine baada ya kuungua soko, walishindwa kuendelea, na hata wale walioendelea bado wanakabiliwa na mikopo mbalimbali, hivyo si rahisi kuhamia hapo kwa haraka kama watu wanavyodhani.
Wabeba mizigo, wauza makufuli
Wakati baadhi ya wafanyabiashara wakilalamikia gharama za kuhamishia bidhaa zao katika Soko Kuu la Kariakoo, kwa wabeba mizigo na wauza makufuli hali hiyo imegeuka kuwa fursa ya kujipatia kipato.
Baadhi ya fremu zilizopo katika Soko Kuu la Kariakoo. Soko hilo lilifunguliwa rasmi jana Februaei 8, 2026 na Rais Samia Sulubu Hassan, baada yakufanyiwa ukarabati mkubwa.
Hamis Lile, mbeba mizigo, amesema leo amejipatia kipato ambacho hakukitarajia, akieleza mpaka saa 10 jioni alikuwa amepata Sh30,000, tofauti na siku za nyuma.
Naye Akbar Rahim, muuza makufuli, amesema kuanza kwa biashara sokoni hapo kumekuwa neema kwake kutokana na ongezeko la mahitaji ya makufuli miongoni mwa wafanyabiashara waliokuwa wakihitaji kufungia vizimba vyao ili kulinda bidhaa.
“Huwa nauza makufuli, lakini leo nimeuza sana. Nilikuja na mzigo mdogo ukaisha, ikabidi nikaongeza tena. Wanasema usiposhukuru kwa kidogo, hata kwa kikubwa hutashukuru,” amesema Rahim.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, Simda Mainga amesema amefurahishwa na kurejea kwa biashara katika soko hilo baada ya takribani miaka minne ya kufanya shughuli zao katika mazingira magumu.
Simda amesema katika saa chache tangu apange bidhaa zake amepata Sh20,000, hali inayompa matumaini kuwa biashara itaendelea kuwa nzuri zaidi siku zijazo.
“Tunashukuru kukamilika kwa soko hili, kwani kwa miaka minne tumeishi katika hali ngumu sana, mvua na jua vilikuwa sehemu ya maisha yetu. Leo tunaona matunda ya uvumilivu wetu, tunaishukuru Serikali,” amesema Simda, mfanyabiashara wa nyanya.
Kwa upande wake, Ibrahim Chagila, ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara wa kwanza kupanga bidhaa zake katika sakafu ya pili, amesema aliwasili sokoni saa 11:00 alfajiri kutokana na hamu kubwa ya kuanza biashara katika soko hilo jipya.
Mmoja wafanyabiashara akiwa anapanga bidhaa kwenye duka lake katika Soko Kuu la Kariakoo.
Hata hivyo, amesema hadi kufikia saa nne asubuhi walizuiwa kuingia na askari mgambo, huku baadhi ya barabara zikiwa zimefungwa kwa mabati, hali iliyowalazimu kushusha bidhaa mbali na soko, hivyo kuingia gharama za ziada za kuwalipa wabeba mizigo.
Ameongeza kuwa baada ya meneja wa soko kufika eneo hilo, aliomba radhi kwa usumbufu uliotokea na kuwaelekeza wafanyabiashara kuanza kuingia, huku mkandarasi akiendelea na kazi ya kuondoa mabati yaliyokuwa yamewekwa.
Naye Rajabu Nuru amesema wana kila sababu ya kushukuru kufikiwa hatua hiyo, akieleza kuwa wakati soko likiwa katika ukarabati, baadhi ya wafanyabiashara walifariki dunia, huku wengine wakiendelea kuugua kutokana na mshtuko walioupata wakati wa ajali ya moto.
Hata hivyo, Nuru ameomba Serikali kuhakikisha kuwa baada ya kufunguliwa kwa soko hilo, hakutakuwa na wafanyabiashara wanaoruhusiwa kufanya biashara nje au barabarani, akisema hali hiyo inaweza kuathiri biashara za walioko ndani na kwenye ghorofa za juu.
“Tunaomba kama bado kuna nafasi ndani ya soko, wafanyabiashara wote wapewe vizimba ili tufanye biashara kwa pamoja. Hii ndiyo njia ya kujenga uchumi wa nchi na kuwapatia wananchi fursa za akujiajiri,” amesema Nuru.