Walemavu 110 kukutanishwa Kilimanjaro usiku wa ‘Night to shine’

Moshi. Wakati jamii ikitakiwa kuwaibua na kutowaonea aibu watu wenye ulemavu nchini,   Shirika la New Life Foundation mkoani Kilimanjaro limepanga kuwakutanisha walemavu 110 mkoani humo kama ishara ya kuwathamini na kuwatambua.

Katika siku hiyo maalumu iliyopewa jina “Night to Shine” ambayo itafanyika Februari 13, 2026, watavalishwa mataji maalumu kama ishara ya kuthaminiwa katika jamii, na kufanya siku yao hiyo kuwa ya kipekee na yenye thamani kubwa.

Akizungumza leo Februari 9, 2026 umuhimu wa kukutana na watu hao wenye ulemavu, rais wa taasisi hiyo, Askofu Glorious Shoo amesema kukutana na watu hao ni kuwaonyesha upendo na kwamba jamii inawathamini kama walivyo watu wengine.

“Night to shine ni mpango wa kimataifa ulioanzishwa na Taasisi ya Team Tibo kwa ajili ya kuonyesha thamani, heshima na utu wa watu wenye ulemavu

“Tumeandaa tukio hili ambalo linajulikana kama ‘Night to shine’ ni usiku ambao umepewa upekee kwa ajili na kuwatambua watu waliopata ulemavu ambapo wanaume wanavikwa kifalme na wanawake watavikwa kimalkia na watapita kwenye zulia jekundu,” amesema Shoo.

Amesema: “Tukio hili ni muhimu sana kwa hawa watu wenye uhitaji maalumu kwa sababu  hawataweza kuolewa, kuoa wala kuhitimu na hawatakuwa na siku yao muhimu kama sisi tunavyofanya, ndio maana tumesema tufanye tukio hili muhimu.”

 “Watu wengi walikuwa wanaona aibu ya kujitambulisha kwamba wana mtoto mwenye ulemavu na kuwaficha ndani, ulemavu sio wa kujitakia, maana mtu yoyote anaweza kuamka akiwa mlemavu,” amesema Shoo.

Naye, mratibu wa shughuli hiyo, Gerald Simon amesema katika tamasha hilo litawakutanisha watu 330 wakiwemo wenye ulemavu 110.

Amesema watu 220 ni wale watakaoambatana na wenye ulemavu na watakaowapokea katika sherehe hiyo.