Dar es Salaam. Baada ya malalamiko ya muda mrefu kuhusu wahitimu kukosa ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira, mpango mpya wa Serikali wa kuunganisha taasisi za elimu ya juu na viwanda umeibua matumaini mapya miongoni mwa wadau wa ajira na uzalishaji.
Wadau hao wamesema kwa muda mrefu kumekuwapo pengo kati ya elimu inayotolewa vyuoni na ujuzi unaohitajika kwenye uzalishaji, hali iliyosababisha waajiri kutumia muda na rasilimali nyingi kuwafundisha wafanyakazi wapya kabla ya kuanza kazi kikamilifu.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Februari 9, 2026 wakati wa uzinduzi wa mpango wa pamoja wa ushirikiano kati ya vyuo na viwanda, uliofanywa na Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi.
Mkurugenzi wa Emirate Aluminium & Glass Co Ltd, Deogratius Marandu, amesema kampuni hiyo kwa muda mrefu imekuwa ikilazimika kuwafundisha waajiriwa wake kutokana na kukosekana kwa mtaala unaofundisha ujuzi wa uzalishaji wa bidhaa za aluminium.
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi, akiwa na viongozi mbalimbali katika picha ya pamoja na baadhi ya waajiri, mara baada ya kuzindua Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Viwanda katika hafla iliyofanyika leo Februari 9, 2026 kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
“Hakuna mtaala unaofundisha kuhusu aluminium hii ikawa inatulazimu kuwafundisha tunaowaajiri na ilikuwa inatupotezea muda. Baada ya kuona changamoto hiyo, tukaingia kwenye ushirikiano na Veta ili wawafundishe vijana, halafu sisi tuwachukue kutokea hapo,” amesema Marandu, akisisitiza mpango wa Serikali ukitekelezwa vizuri utapunguza gharama kwa waajiri na kuongeza tija kazini.
Kwa upande wake, mmiliki wa viwanda vya sukari vya Kagera na Mtibwa, Seif Seif, amesema uwekezaji kwenye rasilimali watu unapaswa kupewa kipaumbele ili kukabiliana na changamoto ya ajira na kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani.
“Sisi tuna utaratibu wa kuchukua wanafunzi vyuoni, tuna programu maalumu ya kuwafundisha na tunawaajiri. Tunatamani tufanye hili kwa ukubwa zaidi, lakini hilo litawezekana endapo tutawekewa mazingira wezeshi na rafiki,” amesema Seif.
Ameongeza ni matarajio ya wadau wengi kuona mpango huo ukitekelezwa kwa vitendo ili wananchi washuhudie mapinduzi yatakayowanufaisha vijana na kuchangia kwa pamoja kutatua tatizo la ajira nchini.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanzania Startup Association (TSA), Zahor Muhaji, amesema mafanikio ya mpango huo yatategemea kwa kiasi kikubwa mazingira yatakayowezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kutoa mafunzo kwa vitendo.
“Kama tunataka utekelezaji wa mpango huu ufanikiwe, lazima kuwe na motisha. Kwa mfano, mwajiri akiwekeza fedha zake kutoa mafunzo kwa vitendo kwa mwanafunzi, apewe nafuu ya kodi,” amesema Muhaji.
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi, akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Viwanda katika hafla iliyofanyika leo Februari 9, 2026 kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Amesisitiza pia umuhimu wa walimu wa vyuo kwenda kujifunza kwenye tasnia ili waelewe mahitaji halisi ya soko la ajira, akieleza kuwa kwa sasa mfumo wa kupata walimu unawajumuisha zaidi wale waliobaki chuoni bila uzoefu wa moja kwa moja wa soko.
Muhaji amewataka pia wadau wa sekta binafsi kushiriki kufundisha vyuoni, hatua aliyoitaja itasaidia kuhamisha uzoefu wa vitendo kwa wanafunzi na kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi unaohitajika katika uchumi wa sasa.
Akizungumza wakati uzinduzi wa mpango huo, Dk Nchimbi amesema ushirikiano baina ya taasisi za elimu na viwanda kwa sasa ni hitaji la lazima.
“Katika dunia ya leo vyuo haviwezi kubaki kuwa visiwa vya nadharia na viwanda haviwezi kukua bila nguvu kazi yenye ujuzi wa soko. Sekta ya viwanda inategemewa sana katika mapitio ya mitaala, utoaji wa mafunzo kwa vitendo, uanagenzi na kusaidia ujuzi unaohitajika sasa na baadaye,” amesema.
Kufanikisha hilo, Dk Nchimbi ametoa maelekezo kadhaa ikiwemo sekta binafsi kushirikiana na vyuo kuwekeza kwenye tafiti hususani za kisayansi na teknolojia pamoja na kuhimiza ubunifu na ujifunzaji.
“Kupitia mpango huu sekta binafsi inaweza kuchangia kwa kufadhili tafiti na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa fani mbalimbali kulingana na mahitaji ya soko la ajira,” amesema.
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi leo Februari 9, 2026 akizindua Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Viwanda katika hafla iliyofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Pia ameelekeza sekta binafsi kutoa fursa za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na waajiriwa wa fani mbalimbali.
Kando na hilo amezitaka taasisi za elimu na sekta binafsi nchini kuzingatia maendeleo ya sayansi na teknolojia katika utekelezaji wa mpango huo ili kuwezesha vijana wa Kitanzania kushindana na kupata nafasi za ajira ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Miongoni mwa wanufaika wa ushirikiano kati ya elimu na viwanda ni Amina Jerome mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) ambaye kwa sasa ni mtaalamu wa kilimo cha miwa.
Amina amesema kiwanda cha sukari cha Mtibwa kiliwachukua wanafunzi na kuanza kuwapa mafunzo yaliyomfanya kubobea kwenye kilimo hicho na sasa ni mwajiriwa.
“Nilibahatika kuwa miongoni mwa waliochaguliwa, nashukuru ushirikiano huo umeniwezesha kufika hapa nilipo leo.
Nitoe wito kwa vijana wenzangu tuwe tunazitumia vyema hizi nafasi za mafunzo kwa vitendo, ukifanya uzembe utawaharibia wanaokuja baada yako, ukweli ni kwamba tunahitaji sana kujifunza kuendana na soko la ajira,” amesema.
Kwa upande wake, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (Must), Yohana Lucas amelalamikia uwepo wa waajiri wanaokataa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo.
“Naamini mpango huu utakwenda kutatua changamoto hii, bado kuna waajiri wanakataa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa kile wanachoona kumfundisha mwanafunzi ni kama kupoteza muda,” amesema Lucas.
Akizungumza kwa niaba ya Bunge, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko amesema kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala kuwa mfumo wa elimu umekuwa ukitoa wahitimu wasioajirika kirahisi kutokana na kukosa ujuzi unaohitajika kwenye soko.
“Tutatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha upatikanaji wa sera, sheria na miongozo yote inayohitajika kwenye utekelezaji wa mpango huu na mingine kama hii. Tunataka ujuzi unaohitajika kwenye soko upatikane vyuoni kwa kuwahusisha wadau,” amesema Husna.
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuzinduliwa mpango huo ni utekelezaji wa ahadi alizotoa Rais Samia Suluhu Hassan katika siku zake 100 madarakani. Siku 100 zitatamatika Febrauri 11, 2026.
“Agosti 28 mwaka jana, Rais Samia wakati huo akiwa mgombea urais, kwenye uzinduzi wa kampeni aliahidi endapo ataingia madarakani katika ndani ya siku 100 Serikali yake itaandaa mpango wa kitaifa wa pamoja kati ya vyuo vikuu, vyuo vya kati na waajiri katika kukuza ujuzi na uwezo wa kuajirika kwa wahitimu.
“Siku 100 hazijafika mpango huu tayari umekamilika ukiwa umeandaliwa kwa kushirikisha vyuo na wadau mbalimbali hasa waajiri na wale ambao tayari wana uzoefu wa kushirikiana na vyuo katika kukuza mitaala yetu,” amesema Profesa Mkenda.