Dar es Salaam. Wakati shule zilianzishwa ili kutoa elimu ya kitaaluma kwa watoto, hali imebadilika hivi sasa.
Shule nyingi zikiwamo za bweni, zimegeuka kuwa vituo vya malezi ya watoto, kazi ambayo kiasili ilikuwa ya familia.
Walimu, waliopaswa kuwa wawezeshaji tu, sasa wamebeba mzigo mzito wa kuwa walezi wa tabia, wahudumu wa afya, washauri wa kisaikolojia na hata “wazazi wa muda” kwa watoto wanaoachwa mikononi mwao na wazazi wasiojihusisha kabisa na malezi.
Katika baadhi ya shule, hali ni ya kusikitisha. Mwalimu mmoja wa shule ya msingi jijini Mbeya anaeleza:
“Mzazi anakuletea mtoto wa miaka sita ambaye hajui kujifunga viatu, hajui kujisaidia, na ni mkaidi kupita kiasi. Ukimwambia mzazi aje kwa ajili ya mazungumzo, anasema hana muda eti niko kazini’.”
Hii ni hali inayojirudia kila mara; mzazi anaamini kuwa kumpeleka mtoto shule ni suluhisho la kila kitu.
Wazazi wengi, kwa makusudi au kwa uzembe, wameamua kuiachia shule jukumu la kumjenga mtoto kimaadili, kiakili, kihisia na hata kiafya.
Wanaamini kwamba kulipa ada na michango ya shule kunawapa leseni ya kujiondoa kabisa kwenye malezi. Matokeo yake ni kwamba walimu wamegeuka kuwa “wazazi wa kitaaluma” kazi ambayo ni ya kuchosha na isiyolipwa wala kutambuliwa.
Mfano wa shule za bweni ni wa kutia moyo, lakini pia wa kutia hofu. Watoto wa miaka mitano hadi minane wanapelekwa mbali na familia zao wakiaminishwa kuwa huko ndiko watajengwa.
Lakini, tofauti na matarajio ya wazazi, shule nyingi hazina uwezo wala mazingira ya kumlea mtoto kwa ukaribu unaohitajika katika umri huo.
Na hata kama zingekuwa nazo, walimu si miungu, hawana uwezo wa kuchukua nafasi ya mzazi kwa asilimia mia.
Serikali iliona hitilafu hii na kutoa agizo kwamba watoto wa chini ya darasa la nne wasipelekwe shule za bweni.
Lakini agizo hilo kwangu limeibua swali pana zaidi: kwa nini mzazi amwelekeze mtoto wake mdogo kwa walimu, kisha ajiondoe kwenye majukumu ya kila siku ya malezi?
Tatizo halipo kwenye bweni pekee, bali katika mtazamo potofu wa mzazi kuhusu nafasi ya shule na walimu.
Nayakumbuka maneno ya Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa: “Watoto wadogo wanahitaji kuwa na wazazi wao ili wajifunze tabia, maadili, na upendo wa kifamilia. Shule haziwezi kuwa mbadala wa familia.” Hii ni kauli inayopaswa kufungua macho ya wazazi wote.
Ni dhahiri kuwa walimu wanafanya kazi ngumu kupita kiasi. Mbali na kufundisha, wanakabiliana na watoto wenye matatizo ya kitabia, kisaikolojia, au kiafya, masuala ambayo yalipaswa kuwa yameshashughulikiwa na mzazi kabla mtoto hajafika darasani.
Katika baadhi ya shule, walimu wanalazimika kuchangia chakula kwa wanafunzi walioachwa na wazazi bila mahitaji ya msingi.
Wengine wanalala nao wakati wa maradhi au huzuni, na hata wakati mwingine kuwapigia simu wazazi bila kupokea majibu yoyote.
Katika shule moja ya msingi wilayani Morogoro, mwalimu mkuu alilazimika kumbeba mtoto mdogo hadi hospitali baada ya kuanguka darasani.
Alimpigia mzazi kwa saa mbili bila mafanikio. Baadaye alitumiwa ujumbe mfupi wa maneno ukisema: “Tafadhali nishughulikie mtoto, niko safarini.”
Matukio kama haya yamekuwa ya kawaida na yanadhihirisha jinsi baadhi ya wazazi wanavyojivua majukumu yao kwa makusudi.
Hali hii imechangia pia kuporomoka kwa maadili shuleni. Walimu wengi wanakiri kuwa kazi yao imekuwa ngumu zaidi kwa sababu wanapambana na watoto wasiojua kusema “samahani”, wasiojua kusikiliza, au kukataa kwa heshima.
Na tatizo hili halianzi shuleni, linatoka nyumbani. Watoto hawa hukua bila mipaka, bila mwongozo, na bila mazungumzo ya karibu na wazazi wao.
Ni wakati wa jamii kutambua kwamba malezi si jukumu la walimu. Walimu wana mchango, lakini mzazi ndiye mwalimu wa kwanza na wa mwisho wa mtoto.
Malezi huanzia nyumbani, na shule ni kiendelezo si mbadala. Wazazi hawapaswi kusubiri matatizo ya kitabia ya mtoto yadhihirike shuleni ndipo waanze kulaumu mfumo wa elimu. Badala yake, wajitazame wao kwanza.
Mzazi anayemlea mtoto wake vizuri huifanya kazi ya mwalimu kuwa rahisi na yenye matokeo chanya.
Lakini mzazi anayekwepa jukumu lake huchangia moja kwa moja katika kuchafua tabia za watoto na kuwatwika walimu mzigo usio wa kwao.
Mjadala huu ni wa kitaifa. Unahitaji mjadala wa wazi na wa kweli kuhusu nafasi ya familia katika malezi.
Serikali inaweza kutoa sera, shule inaweza kuweka taratibu, lakini bila mzazi kujitokeza na kushiriki moja kwa moja, mtoto atabaki kutangatanga kati ya ratiba na masharti, akilelewa na mfumo bila moyo.
Katika kikao cha wazazi kilichofanyika shule moja ya msingi mkoani Arusha, mzazi mmoja alisema kwa uchungu: “Nimempeleka mtoto wangu shule bora, lakini sasa ananitukana. Walimu watamrekebisha?” Mwalimu mkuu alimjibu kwa upole lakini kwa ukweli: “Shule inaweza kumfundisha mtoto kusoma, lakini haimfundishi kuheshimu. Heshima inafundishwa nyumbani.”
Maneno haya yanabeba uzito wa kweli. Mzazi ni msingi wa tabia ya mtoto. Malezi si huduma ya kupewa na taasisi, bali ni jukumu la msingi la kila mzazi mwenye dhamira njema kwa kizazi kijacho.
Kabla mtoto hajakutana na mwalimu, tayari ameshakutana na mzazi; kabla hajajifunza kusoma na kuandika, tayari amejifunza kuzungumza, kuishi na kuiga tabia kutoka nyumbani. Hivyo, mzazi anabeba jukumu lisiloweza kuhamishiwa kikamilifu kwa mtu mwingine.
Shule zisigeuzwe kuwa madampo ya kulelea watoto wa wazazi waliochoka kulea. Mwalimu ana jukumu la kufundisha, kuelekeza na kusimamia nidhamu ya kitaaluma, si kuchukua nafasi ya mzazi katika misingi ya malezi ya kila siku.
Wazazi wanaposhindwa kusimamia tabia za watoto wao nyumbani, matokeo yake huonekana shuleni kupitia utovu wa nidhamu, kukosa heshima kwa wakubwa, na kushuka kwa maadili kwa ujumla.
Mwalimu anapolazimika kutumia muda mwingi kurekebisha tabia badala ya kufundisha, elimu yenyewe huathirika. Hii si haki kwa walimu wala kwa wanafunzi wengine wanaotaka kujifunza katika mazingira tulivu.
Shule zibaki kuwa mahali pa elimu, na familia ibaki kuwa msingi wa malezi. Mtoto anayelelewa vyema nyumbani huingia shuleni akiwa tayari kujifunza, kuheshimu mamlaka na kushirikiana na wenzake. Malezi bora nyumbani huirahisishia shule kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi.
Ni kwa kushirikiana tu kati ya wazazi, walimu na jamii ndipo tunaweza kulea kizazi chenye maarifa, heshima na utu. Kila upande utimize wajibu wake bila kisingizio, kwa sababu mtoto wa leo ndiye taifa la kesho.