YASSIN AWAJULIA HALI WAANDISHI WA HABARI MAJERUHI WA AJALI IRINGA

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Daud Yassin, amewatembelea waandishi wa habari waliopata majeraha kufuatia ajali ya gari iliyotokea tarehe 5 Februari 2026 mkoani Iringa.

Ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Idodi, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, wakati waandishi wa habari wakirejea kutoka Idodi walikohudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo hospitalini, Yassin amesema amefarijika kuona hali za afya za majeruhi hao zikizidi kuimarika siku hadi siku.

“Nimefarijika kufika tena hospitali kuwaona ndugu zangu wanahabari ambao walipata ajali hivi karibuni na kuona hali za afya zao zinazidi kuimarika. Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa rehema hii ya uhai,” amesema Yassin.

Ameendelea kuwatakia waandishi hao uponaji wa haraka, huku akisisitiza mshikamano na mchango mkubwa wa wanahabari katika kuhabarisha jamii na kuunga mkono shughuli za maendeleo.