KIUNGO wa Mogbwemo Queens, Mtanzania Zuwena Aziz ‘Zizou’ amesema kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Wanawake Sierra Leone wakiwa kileleni ni jambo lililowaongezea kujiamini na kuwapa nafasi nzuri ya kulitetea taji hilo.
Mogbwemo Queens inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Sierra Leone imeonyesha kiwango kizuri katika mechi za mzunguko wa kwanza ikishinda mechi zote 11 na kukusanya pointi 33 huku anayemfuata akiwa nazo 24.
Akizungumza na Mwanaspoti, Zizou amesema mafanikio hayo ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na wachezaji pamoja na benchi la ufundi, akisisitiza kuwa hakuna mechi iliyokuwa rahisi kwao.
“Nashukuru tumemaliza mzunguko wa kwanza tukiwa kileleni. Ni jambo zuri kwetu kama timu, lakini pia kwa upande wangu binafsi, nikiwa nimecheza mechi nane, si jambo jepesi hata kidogo,” amesema Zuwena.
Kiungo huyo anayejulikana kwa uwezo wa kutoa pasi zenye macho, ameongeza kuwa msimu huu amebadilishiwa majukumu na kwa sasa anatumika zaidi kama beki wa pembeni nafasi inayomlazimu kuwa na nidhamu kubwa ya kiuchezaji.
“Kocha kwa sasa ananitumia kucheza namba mbili kwa sababu ni nafasi ninayomudu kucheza vizuri, lakini muda wowote anaweza kunibadilisha na nikacheza hata kiungo mkabaji.”
Aliongeza kuwa baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, kikosi kimepewa mapumziko ya wiki mbili kabla ya kurejea kujiandaa na mechi za mzunguko wa pili akisema mapumziko hayo yatasaidia kurejesha nguvu na umakini.