Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiendelea kukabiliwa na uhaba wa ujuzi katika sekta za elimu, afya na utawala wa umma, Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) kimeelekeza nguvu zake kwa wahitimu wake walioko katika taasisi za Serikali ili kusaidia kuimarisha mafunzo ya kitaaluma nchini.
Kupitia juhudi hizo, chuo hicho kinalenga kutumia uzoefu na maarifa ya wahitimu wake katika kuhamasisha na kulea kizazi kijacho cha wataalamu watakaosaidia maendeleo ya taifa.
Hatua hiyo imebainishwa Februari 9, 2026, wakati AKU ilipowakutanisha zaidi ya wahitimu 100 nchini katika mkutano wa ngazi ya juu wa wahitimu.
Mkutano huo ulilenga kuwaunganisha tena wahitimu na wanafunzi wa sasa, pamoja na kuimarisha nafasi ya vyuo vikuu katika kuchangia maendeleo ya taifa.
Wahitimu hao, wanaotoka katika fani za elimu, uuguzi, udaktari na taaluma zinazohusiana, kwa sasa wanafanya kazi katika hospitali za umma, shule na halmashauri za manispaa kote nchini.
Akizungumza na gazeti hili leo, Mkurugenzi wa Masuala ya Wahitimu wa AKU, Nuzhat Kamran, amesema ushiriki wa wahitimu ni mkakati wa kukabiliana na changamoto za rasilimali watu nchini.
“Wahitimu wetu tayari wanachangia maendeleo ya Tanzania wakiwa ndani ya taasisi muhimu za umma.
“Kuwarudisha chuoni kunawawezesha wanafunzi kujifunza kupitia uzoefu halisi na kuelewa kinachohitajika kulitumikia taifa kwa ufanisi,” amesema.
Baadhi ya wanafunzi waliohitimu Chuo Kikuu cha Aga Khan( AKU) wakiwa katika picha ya pamoja na pamoja na viongozi wa chuo hicho baada ya kufanya mazungumzo.
Amesema chuo kinaendelea kuimarisha mifumo ya wahitimu ili kuhakikisha ushauri endelevu, mwongozo wa kitaaluma na ushirikiano kati ya wahitimu, wahadhiri na wanafunzi.
Kamran amesema maoni ya wahitimu pia husaidia chuo kulinganisha programu zake na mahitaji ya soko la ajira.
Mmoja wa wahitimu waliozungumza katika mkutano huo, Dk Vumilia Mmari, ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Uhakiki wa Ubora katika Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet), alizitaka taasisi za elimu ya juu kuufanya ushiriki wa wahitimu kuwa sehemu ya kudumu ya kuboresha ubora wa elimu.
“Wahitimu hawapaswi kupotea baada ya kuhitimu masomo.
“Wengi wao sasa wako katika nafasi nzuri ya kusaidia vyuo vikuu kupitia ushauri, uhamishaji wa ujuzi na kuchangia katika taasisi ambazo mahitaji yake ni makubwa,” amesema.
Amesema ushiriki wa wahitimu unaweza kusaidia kukabiliana na mapungufu ya muda mrefu katika ubora wa ufundishaji, uzoefu wa kitaaluma na maandalizi ya wanafunzi, hususan katika vyuo vikuu vya umma.
Wataalamu wanasema mbinu ya AKU inaonesha kwa uwazi nafasi inayozidi kuwa muhimu ya taasisi za elimu ya juu nchini Tanzania, ambako ukosefu wa ajira kwa vijana na kutolingana kwa ujuzi bado ni changamoto kubwa.
Mchambuzi wa sera za elimu, Joyce Neligwa, amesema ushiriki wa wahitimu unaimarisha uwajibikaji na umuhimu wa elimu ya vyuo vikuu.
“Wahitimu wanaporejea kushirikisha uzoefu wao, husaidia taasisi kuelewa kinachoendelea katika mazingira halisi ya kazi.
“Hii huboresha ubora wa mafunzo na kuhakikisha wahitimu wanajiandaa vyema kwa huduma za umma,” amesema.
Amesema katika sekta ya afya, wahitimu wa AKU wamekuwa sehemu muhimu ya nguvu kazi, hususan katika hospitali za umma na zile za taasisi za kidini.
Mtaalamu wa mifumo ya afya, Dk Ahmed Rashid, amesema wahitimu wa chuo hicho wanatambulika kwa taaluma na maadili ya kazi.
“Wahitimu wa AKU wanaonekana wazi katika hospitali za wilaya na programu za afya kote nchini. Mchango wao unaimarisha utoaji wa huduma katika maeneo yanayokabiliwa na uhaba wa wataalamu wenye ujuzi,” amesema.
Amesema katika mkutano wa Dar es Salaam, wahitimu walishirikisha uzoefu wao wa kufanya kazi katika jamii zisizopata huduma za kutosha, kusimamia taasisi za umma na kukabiliana na changamoto za maendeleo ya ndani.
Dk Rashid amesema kwa wanafunzi wa sasa, muingiliano huo umewapa fursa ya kuona kwa karibu njia za ajira katika huduma za umma.