‘DED’ Kigoma Ujiji, wenzake waliohukumiwa miaka 20 waachiwa

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Kigoma imewaachia huru aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji (DED), Athumani Msabila na aliyekuwa mhazini wa halmashauri hiyo, Frank Nguvumali, waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.

Msabila na mwenzake walikutwa na hatia ya makosa mawili ambayo ni kughushi nyaraka na utakatishaji fedha.

Msabila na wengine 10 wakiwemo maofisa kutoka Idara ya Fedha ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, walishtakiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo kughushi nyaraka kwa nia ya kudanganya kuhusu matumizi ya fedha za umma ikiwemo zilizotengwa kwa ajili ya mafunzo na miradi ya maendeleo, na utakatishaji fedha Sh463.5 milioni.

Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa ni Aidan Mponzi, Tumsifu Kachira, Ferdinand Filimbi, Salum Saidi, Moses Zahuye, Joel Shirima, Jema Mbilinyi, Kombe Kabichi na Bayaga Lucas.

Katika kesi ya msingi, Msabila na wengine waliokutwa na hatia na adhabu zao kwenye mabano ni Filimbi (2), Saidi (2), Nguvumali (miaka 22) na Lucas (2). Walioachiwa huru baada ya kukutwa hawana hatia katika shauri hilo ni Mponzi, Kachira, Zahuye, Shirima, Mbilinyi na Kabichi.

Msabila, Filimbi, Saidi na Nguvumali walikata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma ambapo uamuzi uliowaachia huru umetolewa jana, Jumatatu Februari 9, 2026, na Jaji John Nkwabi.

Jaji amesema Mahakama baada ya kupitia mwenendo, sababu za rufaa na hoja za pande zote mbili, ilikubaliana na hoja za warufani kwamba upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya warufani kwa kiwango kinachotakiwa kisheria cha bila shaka yoyote.

Mahakama hiyo ilifuta hukumu na adhabu zilizotolewa dhidi ya warufani katika shtaka la kwanza la kughushi chini ya vifungu vya 333, 335(a) na 337 vya Kanuni ya Adhabu.

Vilevile, hukumu na adhabu zilizotolewa dhidi ya warufani katika shtaka la saba la utakatishaji fedha chini ya kifungu cha 12(1)(d) na 13(1)(a) cha Sheria ya Kupambana na Utakatishaji Fedha zilifutwa.

Jaji amesema Mahakama imejiridhisha vielelezo muhimu vilivyotegemewa na upande wa mashtaka, hususani maelezo ya onyo na ripoti za ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), vilipatikana na kupokelewa kinyume cha sheria na havina thamani ya ushahidi wa kuweza kuunga mkono hukumu za hatia.

Amesema maelezo ya onyo yaliyotegemewa na upande wa mashtaka yalirekodiwa nje ya muda unaoruhusiwa kisheria na mazingira ambayo mtuhumiwa alitoa maelezo hayo hayakuthibitishwa kuwa yalikuwa ya hiari.

Mahakama ilibaini mtuhumiwa alikaa kizuizini kwa muda mrefu bila kupatiwa mahitaji ya msingi, hali iliyoathiri uhuru wake wa kisaikolojia. Mahakama ikaamua kuyaondoa maelezo hayo ya onyo kwenye kumbukumbu za kesi na kuyakataa kama kielelezo.

Aidha, Mahakama hiyo ilifuta vielelezo muhimu vilivyokuwa vinaunga mkono kesi hiyo, ambavyo ni maelezo hayo ya onyo na ripoti ya ukaguzi ya CAG, baada ya kubaini haikufuata misingi ya kitaalamu ya ukaguzi wa fedha za umma.

Mahakama ilisisitiza ripoti ya kitaalamu haiwezi kusimama peke yake bila kuungwa mkono na ushahidi wa msingi kama vile nyaraka za benki, hati za uhamishaji wa fedha, stakabadhi za malipo na vielelezo vya makabidhiano ya fedha taslimu.

Kesi hiyo ilihusisha madai ya upotevu wa kiasi cha Sh27.4 milioni kutoka katika akaunti za Manispaa ya Kigoma Ujiji katika kipindi cha Desemba 2022 hadi Januari 2023.

Kumbukumbu za hukumu hiyo zinaeleza Septemba 20 na 21, 2023, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa ziarani mkoani humo, alibaini kuhusu ubadhirifu wa fedha katika halmashauri hiyo.

Ili kuthibitisha madai hayo, Oktoba 5, 2023 aliunda kamati maalum iliyochunguza tuhuma hizo, ambapo matokeo ya uchunguzi huo hayakuwasilishwa mahakamani hapo.

Ilidaiwa kupitia kwa Katibu wake, Raymond Bowele, Oktoba 27, 2023 Waziri Mkuu alimuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum wa hesabu za miamala na matumizi ya serikali ya Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Kabla ya ukaguzi, katika tarehe tofauti, washtakiwa hao 11 walikamatwa, kuhojiwa na kufikishwa mahakamani Novemba 7, 2023 katika Mahakama ya Wilaya ya Kigoma ambapo baadaye kesi hiyo ilifutwa na Machi mosi 2024 walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na makosa manane.

Katika kosa la kwanza lililokuwa likimkabili Msabila, Filimbi, Saidi na Nguvumali ni kughushi kinyume na vifungu vya 333, 335(a) na 337 vya Kanuni ya Adhabu.

Ilielezwa Desemba 28, 2022 kwa nia ya kudanganya walighushi hati iliyokuwa na jina la “maombi ya kutumia Sh42.4 milioni kwa ajili ya mafunzo ya siku tano ya mfumo wa bajeti (PLANREP na FFRAS)”.

Shtaka la pili lililokuwa likiwakabili Shirima, Mbilinyi na Kabichi ni kughushi ambapo ilielezwa Juni 5, 2023 katika Mkoa wa Kigoma, kwa nia ya kudanganya walighushi hati yenye jina la “ripoti ya ukaguzi” ikionyesha skip buckets tisa zenye thamani ya Sh18 milioni zilipelekwa katika halmashauri hiyo wakijua si kweli.

Shtaka la saba lilikuwa ni utakatishaji fedha kinyume na kifungu cha 12(1)(d) na 13(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia Utakatishaji Fedha, ikisomwa pamoja na kifungu cha 60(2) cha Sheria ya Udhibiti wa Uhalifu wa Kiuchumi na Kupangwa.

Katika shtaka la nane, washtakiwa walituhumiwa kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh129.4 milioni.

Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 20 na vielelezo 29.