MCHEZAJI Bora wa Ligi Kuu Bara kwa Januari, William Edgar wa Dodoma Jiji amesema japo kila mechi wanayocheza kwa sasa ni kama fainali, lakini anatamani kumaliza msimu huu akiwa amefunga si chini ya mabao 10 ili kuweka heshima n rekodi binafsi katika Ligi Kuu.
Edgar aliyemaliza na mabao sita na asisti nne na mechi za mtoano alifunga mabao mawili msimu uliyopita, akiwa na Fountain Gate amesema anatamani kuandika rekodi mpya katika ufungaji.
“Japo wakati nikiwa FG tulicheza mechi za mtoano ili tusishuke daraja, lakini ulikuwa msimu mzuri kwangu na msimu huu nimefunga mabao manne, ndio maana natamani angalau nifunge kuanzia 10,” amesema Edgar na kuongeza:
“Ugumu wa ligi unasaidia ushindani kuanzia kwenye namba hadi tukicheza na wapinzani pia unapandisha kiwango cha mchezaji anayejituma kwa bidii.”
Hata hivyo nyota huyo wa zamani wa Mbeya Kwanza na KenGold aliwahi kutwaa tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi ya Championship ikiwamo wakati anaipandisha Ligi Kuu KenGold misimu miwili iliyopita alipofunga mabao 21.
Mbali na malengo binafsi, amesema anatamani kuona Dodoma Jiji inamaliza ikiwa nafasi za juu katika msimamo wa ligi.