Elimu kikwazo walio pembezoni kuwekeza soko la hisa

Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakianza kuchangamkia uwekezaji katika masoko ya hisa na hatifungani, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeeleza uelewa mdogo wa masuala ya kifedha ndio unaofanya mikoa mingine kubaki nyuma, huku Dar es Salaam ikiendelea kuongoza kwa idadi ya wawekezaji.

Hayo yameelezwa leo Jumanne, Februari 10, 2026 na Mkuu wa kitengo cha Uchambuzi wa Soko, Ufuatiliaji na Usimamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mlekwa kulwa wakati akifungua mashindano ya utafiti katika soko la hisa ya vyuo vikuu yajulikanayo kama CFA Institute Research Challenge Local Finals kwa mwaka 2025/2026.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kulwa amesema ukuaji wa idadi ya watu wanaowekeza katika soko la hisa ni jambo jema kwa nchi huku akilinganisha na miaka michache nyuma ambayo watu walikuwa hawajahamasika kutumia ipasavyo masoko ya fedha.

“Ni jambo jema kwani DSE (Soko la Hisa la Dar es Salaam) inakuwa kubwa na watu wengi wanashiriki. Pia sisi kama BOT tunashughulikia ujumuishaji huduma za kifedha, wanapowekeza huku wanafanya diversification (uwekezaji katika maeneo mbalimbali ili kupunguza hatari na kuongeza fursa za kupata faida),” amesema.

“Hii inaonyesha kuwa si lazima ulime bali ili upate hela bali unaweza kuwekeza katika hisa faida utakayoipata utaitumia kufanya shughuli nyingine,” amesema.

Licha ya kukua kwa uwekezaji huo, Kulwa anabainisha kuwa mwamko ni mkubwa sana kwa upande wa Dar es Salaam huku baadhi ya wakazi wa mikoani wakiwa hawajui kuhusu fursa hiyo.

“Benki Kuu imepiga hatua katika kuongeza uelewa huu, kuna kurugenzi mahususi ambayo inahusika na suala hili inayozunguka Tanzania nzima ikifanya mambo mbalimbali yanayochagiza wananchi wafahamu mambo ya fedha na sasa wanaandaa watoa elimu ya fedha kwa jamii (CFA), ili kuongeza hamasa na ufahamu katika mambo ya fedha na masoko ya fedha,” amesema.

Kwa mujibu wa takwimu za uwekezaji kutoka soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa idadi ya akaunti za uwekezaji zilizosajiliwa, ukiwa na akaunti 36,636 sawa na asilimia 38.64, ukifuatiwa na Mkoa wa Arusha wenye akaunti 6,278 sawa na asilimia 6.62.

Akizungumzia shindano la wanafunzi kutoka vyuo vikuu amesema inawasaidia kufahamu kwa undani juu ya masoko ya fedha na kuwajengea uwezo wa kuyachambua ili waweze kuwa washauri wazuri kwa watu wanaotaka kufanya uwekezaji kwa kuwaonyesha ni sehemu gani sahihi.

“Katika kukuza uelewa wa soko la hisa zoezi ni muhimu kwani linajenga watu wanaojua kuchambua masoko ya fedha na hisa na kutoa ushauri ni sehemu gani wananchi wanaweza kuwekeza, kwani wanaweza kufahamu hali halisi na maono ya baadaye kwa kila kampuni kwa kuangalia inaweza kukua kwa kiasi gani, kushuka au kubaki ilipo,” amesema.

Amesema hiyo itawasaidia kuwa washauri wazuri na kupata uhalisia wa kile kilichopo sokoni kwani wanaposoma vyuoni wanaweza wasipate uhalisia, lakini wakiingia sokoni wanaweza kuona utofauti wa kile walichokisoma darasani kinavyotumika sokoni.

Akielezea wanafunzi hao walivyopatikana, Msimamizi mkuu wa CFA Tanzania, Lucy Shantiwa amesema mashindano hayo yalihusisha wanafunzi kutoka vyuo vyote Tanzania lakini ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mzumbe, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo cha Usimamizi wa fedha (IFM) ndiyo walijitokeza kushiriki.

Amesema programu hiyo hukusanya wanafunzi katika makundi ya watu watano ili waweze kufanya uchambuzi kwa kampuni inayochaguliwa ili kuonyesha namna wanavyoweza kupata faida na upeo wao wanaishauri vipi.

“Tuliwakusanya kwa muda wa miezi sita, wakasaidiwa na wataalamu wa soko husika, kutoka BoT, NMB na kuwaelekeza namna ya kuandaa mawasilisho yao na kujibu maswali yao, mwanzoni tulikuwa na washiriki 300 na hadi tunafikia hatua hii wamebakia 70,” amesema.

Mkuu wa Idara ya Masoko, Rahma Mwapachu amesema mashindano hayo ni jukwaa linalowaandaa viongozi wa baadaye wa sekta ya fedha kwa kuwajengea msingi wa umahiri wa kiufundi ulioimarishwa na maadili na nidhamu.

Hilo litachochea kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu kupitia huduma za kifedha zenye uwajibikaji na zenye umuhimu kwa jamii.

“Mwaka huu ni wa kipekee kwetu kwani kwa mara ya kwanza, washiriki kutoka nchi za Afrika Mashariki zikiwamo Kenya, Uganda, Ethiopia na kwingineko wanaitumia NMB kama kampuni lengwa katika tafiti zao. Tunachukulia hili kama heshima kubwa na pia hatua muhimu ya kimkakati,” amesema.

“NMB  tunawekeza makusudi kwa kizazi kijacho. Kupitia programu za mafunzo ya vitendo (internships), programu za mafunzo ya uongozi (management trainee programmes), na mipango ya ukuaji wa taaluma kwa vijana, tunalea vipaji vyenye mizizi ya maadili, umahiri, na tamaa ya mafanikio. Uwezo ulio ndani ya ukumbi huu leo unaonekana wazi.”