AZAM FC imewasapraizi mashabiki wa soka nchini baada ya kuvuna alama nyingi zaidi kuliko timu nyingine zote zinazoiwakilisha nchi katika michuano ya CAF, licha ya kushiriki makundi kwa mara ya kwanza na sasa inasaka tiketi ya robo fainali.
Timu hiyo itaifuata Wydad AC ya Morocco katika mechi ya mwisho ya Kundi B ya Kombe la Shirikisho ambapo kama itashinda ugenini itaiweka pazuri kuungana na wenyeji, japo itaomba AS Maniema ya DR Congo ipoteze au kutoka sare nyumbani dhidi ya Nairobi United ya Kenya.
Hata hivyo, licha ya hesabu kuonekana kuwa ngumu kwa Azam, kocha wa timu hiyo Florent Ibenge amekula kiapo kwa kusema mshabiki wa klabu hiyo watulie tu, kwani Wydad hata kama ipo nyumbani bado inafungika kabisa.
Ibenge amesema ni kweli mechi hio inaonekana ni ngumu kwa Azam kupata ushindi ugenini, lakini wao wanakwenda na hesabu kali, huku akiwapongeza mastaa wa kikosi hicho kwa kazi kubwa waliyoifanya hadi sasa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge amesema, mchezo unaofuata unaonekana kuwa mgumu kwao, lakini hiyo ni picha ya nje tu, ila ndani ya kikosi hicho wamejipanga kuhakikisha hawakati tamaa wala kuogopa.
Amesema, bado wana matumaini ya kufanya vyema kutokana na aina ya wachezaji wenye ubora wa kubadili matokeo wakati wowote wanapokuwa mchezoni.
“Yapo mambo mengi ambayo yanatupa morali na uhakika wa kufanya vyema kwenye mchezo unaofuata, hii haimaanishi tunawadharau wapinzani wetu, hapana. Tunakwenda kukutana na Wydad ambayo imeshaatangulia kukata tiketi ya kwenda robo, hivyo utakuwa uamuzi wa Azam na wachezaji pekee kusaka matokeo ya ushindi,” amesema Ibenge na kuongeza:
“Lakini nawapongeza wachezaji kwa kuendelea kucheza kwa hesabu nzuri na kupata matokeo. Naamini kabisa safari hii ya makundi tutaimaliza kwa ushindi.”
Kwa sasa Azam inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tisa kama ilizonazo Maniema ikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa tu, wakati Nairobi United ikiwa inaburuza mkia wa kundi bila pointi yoyote hadi sasa licha ya kucheza mechi tano.
Wydad itakayokuwa nyumbani kuialika Azam, Jumapili ya Februari 15, tayari imeshafuzu robo fainali kutokana na kumiliki pointi 12 baada ya mechi tano na katika mechi ya awali baina ya timu hizo Wanalambalamba walipasuka bao 1-0 nyumbani Amaan Complex, Z’bar.