JAMII YAONYWA KUZINGATIA KANUNI ZA MATUMIZI SALAMA YA INTANETI

……

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Serikali imewataka  watumiaji wote wa mitandao nchini kufuata taratibu na kanuni za matumizi salama ya intaneti ili kujikinga na madhara yanayotokana na matumizi mabaya ya teknolojia.

Wito huo umetolewa leo Februari 10, 2026 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Nicholous Merinyo Mkapa, aliyemwakilisha Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, katika maadhimisho ya 22 ya Siku ya Usalama Mtandaoni yaliyoadhimishwa sambamba na nchi zaidi ya 190 duniani.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Dkt. Mkapa alisema kukua kwa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), pamoja na kuibuka kwa Akili Unde (AI), kumeleta fursa nyingi katika elimu, biashara, mawasiliano na huduma za kifedha, lakini pia kumeongeza hatari za uhalifu wa mtandaoni.

“Mtandao hauna mipaka ya kuzuia watu wenye nia ovu. Kumekuwepo na vitendo vya ulaghai, utapeli na udukuzi wa taarifa binafsi. Ni muhimu wanafunzi na watumiaji wote kuzingatia kanuni za usalama mtandaoni ili kujilinda na kulinda wengine,” alisema Dkt. Mkapa.

Alisisitiza kuwa usalama mtandaoni ni jukumu la kila mmoja, akihimiza wazazi, walimu, taasisi za elimu na watoa huduma za mawasiliano kushirikiana katika kutoa elimu ya matumizi sahihi ya intaneti.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabir Bakari, alisema maadhimisho ya Siku ya Usalama Mtandaoni, yaliyoanzishwa mwaka 2004, yanalenga kuhamasisha matumizi salama na kuwajengea uwezo watumiaji kukabiliana na changamoto zinazoibuka katika ulimwengu wa kidijitali.

Alisema TCRA imeanzisha Vilabu vya Kidijitali (Digital Clubs) katika shule za msingi, sekondari na vyuo ili kuwajengea vijana uelewa wa usalama wa mifumo ya TEHAMA na kukuza ubunifu.

Aidha, kupitia mashindano ya kila mwaka ya Cyber Champion Competition, wanafunzi wa vyuo vya serikali na binafsi hujengewa uwezo wa kiufundi katika masuala ya usalama mtandaoni. 

Mwaka huu, shindano la sita limehusisha washiriki kutoka vyuo mbalimbali, ambapo washindi walipatikana Januari 29 na kutunukiwa zawadi zikiwemo kompyuta mpakato.

Naye Mwakilishi wa Kamati ya Taifa ya Ushauri kuhusu Usalama wa Mtoto Mtandaoni, Mwelide Kato, alisema tafiti zinaonesha kuwa asilimia 67 ya watoto wenye umri wa miaka 12 hadi 17 wanatumia mitandao, huku asilimia 4 wakiripotiwa kukumbana na ukatili wa mtandaoni.

Alisema serikali imezindua kampeni ya kitaifa ya kuelimisha wazazi na walezi kuhusu namna ya kuwalinda watoto wanapotumia mitandao, sambamba na kuimarisha mifumo ya kisheria dhidi ya makosa ya kimtandao.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni:

“Teknolojia Mahiri, Chaguo Salama: Tuwalinde Watoto katika Zama za Akili Unde.”

Siku ya Usalama Mtandaoni huadhimishwa kila Jumanne ya pili ya mwezi Februari kila mwaka kwa lengo la kuongeza uelewa wa matumizi sahihi ya intaneti na kujenga jamii salama katika dunia ya kidijitali.