Arusha. Kuanza kwa jimbo jipya la Kanisa Katoliki ni sawa na kupanda mbegu kwenye ardhi mpya; huhitaji maono, uvumilivu na uongozi thabiti ili liote na kuzaa matunda. Hilo ndilo jukumu linalomsubiri Askofu Mteule Prosper Balthazar Lyimo, Askofu wa kwanza wa Jimbo jipya la Katoliki la Bariadi, aliyeteuliwa Januari 8, 2026 na Baba Mtakatifu Leo XIV.
Askofu Lyimo anakabidhiwa jimbo changa lenye mahitaji makubwa ya kichungaji, kiutawala na kimaendeleo, huku akitarajiwa kuweka misingi itakayoliongoza Kanisa hilo kwa vizazi vijavyo.
Katika mahojiano na Mwananchi, amesema ujenzi wa jimbo jipya si suala la majengo pekee, bali ni safari ya kujenga imani, mshikamano na mifumo imara ya utumishi wa Kanisa.
Amesema majukumu yake ya awali ni pamoja na kuimarisha parokia 19 zilizopo, kuendeleza miundombinu ya Kanisa, kusimamia malezi ya majandokasisi 48 na kuendeleza taasisi za elimu na afya zinazomilikiwa na Kanisa katika eneo hilo.
“Jimbo jipya linahitaji msingi imara wa kichungaji unaojengwa juu ya furaha, amani, sala na shukrani. Haki na amani vina thamani kubwa kuliko mali ya dunia,” amesema Askofu Lyimo akisisitiza kuwa Kanisa linapaswa kuwa mahali pa matumaini na mshikamano kwa waamini.
Ameongeza kuwa atahakikisha zinakuwepo jitihada za makusudi kukuza mshikamano wa waamini, kuhimiza wito wa kipadre na kitawa, pamoja na kuwajengea waumini uelewa wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za Kanisa na maendeleo ya jamii yao.
Uteuzi wa Askofu Lyimo unafuatia tangazo rasmi la Baba Mtakatifu Leo XIV la kuundwa kwa Jimbo jipya la Katoliki la Bariadi lililomegwa kutoka Jimbo Katoliki la Shinyanga na kuwekwa chini ya Jimbo Kuu la Mwanza.
Makao makuu ya Jimbo hilo yako mjini Bariadi, ambapo kwa sasa Kanisa Kuu ni Parokia ya Mtakatifu Yohane Mwinjili, huku ujenzi wa Kanisa Kuu jipya la Mtakatifu Luka ukiendelea.
Askofu Lyimo anaendelea kubeba kauli mbiu yake ya kichungaji aliyokuwa nayo tangu akiwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Arusha, inayotokana na 1 Wathesalonike 5:16–18 isemayo: “Furahini siku zote, salini bila kukoma, shukuruni kwa kila jambo.”
Kauli mbiu hiyo inaakisi mwelekeo wa utumishi wake unaojikita katika imani, unyenyekevu na shukrani.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya uteuzi wake, Askofu Lyimo amekiri kuwa haikuwa rahisi kwake kuupokea wito huo mara ya kwanza. Amesema uzito wa jukumu hilo ulimlazimu kusali na kutafakari kwa kina kabla ya kulikubali.
“Haukuwa uamuzi mwepesi, lakini baada ya sala na tafakari niliuona huu kama mpango na mapenzi ya Mungu. Ninaamini Mungu aliyeniumba kwa sura na mfano wake atanitegemeza katika wito huu mpya na kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu kwa uaminifu na uadilifu mkubwa,” amesema.
Ametoa shukrani za dhati kwa waamini wa Jimbo Kuu la Arusha kwa upendo, ushauri na mshikamano waliompa katika kipindi chote cha utumishi wake kama Askofu Msaidizi, akiwataka waamini wa Jimbo Katoliki la Bariadi kumpokea na kushirikiana naye kwa karibu katika kulijenga jimbo hilo changa.
Historia ya Askofu Lyimo inaonyesha safari ndefu ya malezi na utumishi ndani ya Kanisa. Alizaliwa Agosti 20, 1964 katika Kyou-Kilema, Jimbo Katoliki la Moshi. Baada ya masomo ya msingi katika shule za Maua na Arusha, alijiunga na Seminari Ndogo ya Jimbo ya Mtakatifu Tomaso wa Akwino, Arusha.
Alisomea falsafa katika Seminari Kuu ya Kibosho, Moshi, na taalimu ya Mungu katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Paul Kipalapala, Tabora. Alipata daraja la upadri Julai 4, 1997 katika Jimbo Kuu la Arusha.
Katika utumishi wake, amewahi kuwa mlezi wa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Tomaso wa Akwino, Katibu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha, na baadaye kujiendeleza kielimu katika Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana, Roma, na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Paul, Ottawa, Canada, ambako alipata shahada ya uzamivu.
Mnamo Novemba 11, 2014, Baba Mtakatifu Francisko alimteua kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Arusha na kuwekwa wakfu Februari 15, 2015, kabla ya kuteuliwa Januari 8, 2026 kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Bariadi.
Kwa kuanza safari yake kama jimbo changa lenye eneo la kilomita za mraba 16,638 na waamini takribani 366,000 kati ya wakazi 1,221,540, Jimbo la Bariadi linakabiliwa na changamoto za miundombinu, rasilimali watu na fedha.
Hata hivyo, Askofu Lyimo anaona changamoto hizo kama fursa ya kuimarisha imani, mshikamano na ushiriki wa waamini katika kulijenga Kanisa lao.
“Jimbo hili ni letu sote. Nikishirikiana na mapadre, watawa na waamini, ninaamini Bariadi itakuwa mfano wa jimbo linalokua kiimani na kimaendeleo,” amesema.