Al Nasr imefikia makubaliano rasmi na Simba ya kumnunua mshambuliaji Kibu Denis baada ya klabu hiyo ya Misri jana kukubaliana maslahi binafsi na nyota huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Baada ya awali Simba kuonyesha utayari wa kumuuza Kibu Denis, kilichobakia kilikuwa ni makubaliano binafsi baina ya Al Nasr na Kibu Denis ambayo yalichelewa kufanyika kwa vile mchezaji huyo alikuwa Angola akiitumikia Simba katika mchezo wa raundi ya tano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Lakini baada ya nyota huyo kurejea, jana, Jumatatu, Februari 9, 2026, miamba hiyo ya Libya ilikutana na upande wa mchezaji huyo na wakakubaliana rasmi na hivyo mchezaji huyo ataungana na Al Nasr.
Uhamisho huo utaifanya Simba ivune kiasi cha Dola 300,000 (Sh776 milioni) kwa kukubali kumuachia Kibu ambaye mkataba wake ulibakia miezi mitano ufikie tamati.
Msimamizi wa Kibu Denis, Carlos Sylivester amesema kuwa taarifa zozote kuhusu mshambuliaji huyo zitatolewa na Simba.
“Waajiri wa Kibu Denis ni Simba hivyo wao kama kuna lolote linalomhusu mchezaji ndio wanaweza kutoa ufafanuzi,” amesema Sylivester.
Kibu Denis ameitumikia Simba kwa miaka minne na nusu tangu alipojiunga nayo mwaka 2021 akitokea Mbeya City.
Al Nasr inaongoza msimamo wa kundi namba nne la Ligi Kuu ya Libya ikiwa na pointi 21 ilizokusanya baada ya kuibuka na ushindi katika mechi zote saba ilizocheza.
Msimu huu Kibu Denis ameifungia Simba mabao mawili yote yakiwa ni katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mabao hayo aliyafunga katika mechi ya raundi ya kwanza dhidi ya Nsingizini Hotspurs ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Ndani ya Al Nasr, Kibu atakutana na nyota wawili aliocheza nao Simba hivi karibuni ambao ni kiungo Fabrice Ngoma na mshambuliaji Steven Mukwala.