Kipre Junior anusurika panga Algeria

DILI la winga Kipre Junior kuachwa pale MC Alger ya Algeria limebuma baada ya mchezaji huyo aliyekuwa akiwaniwa kubebwa na wapinzani wa Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, FAR Rabat ya Morocco kubaki.

MC Alger ilitaka kumtema Kipre katika dirisha hili dogo ambapo hesabu zilikuwa ni kumnasa winga Nolan Mbemba kutoka Ufaransa.

Mbemba alikuwa akiwaniwa na timu tatu ambazo ni MC Alger, FAR Rabat na timu moja ya Saudia, lakini maafande hao wa Morocco ndio walifanikiwa kuinasa saini kwa dau kubwa ambalo timu zingine zilikwama kulifikia.

Taarifa kutoka Algeria ni kwamba baada ya kutua FAR Rabat, kocha Rhulani Mokwena alifanya uamuzi wa kubaki na Kipre aliyetua katika timu hiyo akitokea Azam FC, huku akimtaka kuonyesha ubora kwenye mechi za kumalizia msimu huu

Mmoja kati ya watu wa karibu wa Kipre Jr ameliambia Mwanaspoti kwa kuwa, “kocha alifanya kikao na Kipre na wamekubaliana kwamba ataongeza bidii, akamuahidi kwamba atampa nafasi ya kucheza kwenye mechi zilizosalia msimu huu.”

Katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika, hatua ya makundi wikiendi iliyopita MC Alger ilishinda nyumbani mabao 2-1 dhidi ya Al Hilal ya Sudan, kocha Mokwena alimpa dakika 29 za kumalizia pambano hilo akichukua nafasi ya Zinedine Ferhat aliyefunga bao moja na kutoa asisti.

Mkataba wa Kipre wakati anatoka Azam ulikuwa na kipengele cha kuwatanguliza matajiri hao wa Chamazi kuwa klabu ya kwanza kupewa nafasi ya kuulizwa kama itataka kumrudisha mchezaji huyo endapo atatakiwa kuondolewa MC Alger.