Unguja. Wakati vijana wakikabiliwa na ukosefu wa ajira, kutokuwa na ujuzi imetejwa kuwa moja ya sababu inayowafanya washindwe kuzifikia fursa na kutimiza ndoto zao.
Azimio la vijana Amani na Usalama 2250 limebainisha maeneo makuu matano ambayo nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wanapaswa kutekeleza maeneo hayo ili kuhakikisha vijana wanaendelezwa na kujengewa uwezo kuepusha migogoro na kukuza uchumi
Maeneo hayo ni ushiriki, ulinzi, uzuiaji, ushirikiano uondoshaji na urejeshaji.
Katika eneo la uzuiaji linasisitiza upanuaji wa uelewa na fursa za kiuchumi kwa vijana kama vile kusaidia fursa za ajira, mafunzo ya ufundi, ujasirimali na kujenga utamaduni wa amani ikiwa ni mojawapo ya uendelezwaji wa mikakati inayolenga kumzuia kijana kutoshiriki katika shughuli za uchafuzi wa amani na kuwa chanzo cha uwepo wa migogoro.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Mwanakwerekwe Februari 10, 2026, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Salhina Mwita Ameir, amesema vijana wakipata ujuzi wanapunguza utegemezi na kujenga uchumi wao.
Jumla ya vijana 30 wamehitimu na kukabidhiwa vyeti katika mafunzo hayo ya vitendo yaliyofadhiliwa na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia mradi wa Dumisha Amani katika fani za ushoni, umeme na ufundi mabomba ambapo wamejifunza kwa vitendo katika maeneo mbalimbali ya viwandani na hotelini.
Naibu katibu mkuu huyo, amewataka vijana kutumia ipasavyo fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kujikwamua kiuchumi.
“Ujuzi kwa vijana unapunguza utegemezi kwao na kwa taifa, maana katika dunia ya sasa inategemea ujuzi, kwahiyo tutumie fursa hii na kuwa mabalozi kwa wengine katika kujikwamua,” amesema
Kadhalika, amewataka vijana kuwa mabalozi wazuri wa kulinda na kudumisha amani ya nchi, akisema kuwa katika nyakati baadhi ya vijana huingizwa katika mikumbo ya kuichafua amani.
Naibu Katibu Mkuu huyo amesema kujiingiza katika matendo ya uvunjifu wa amani hakuchangii maendeleo ya nchi wala ustawi wa wananchi wake, hivyo vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuitunza na kuidumisha amani.
“Msikubali kushawishiwa wala kurubuniwa kwa namna yoyote ile kujiingiza katika matendo yatakayovunja amani ya nchi. Zanzibar ni yenu vijana, na nyinyi ndio walinzi wa amani hiyo,” amesema.
Naye Mwakilishi wa UNDP, Fridah Mwakasyuka, amesema bado vijana wengi wanakabiliwa na tatizo la ajira, changamoto kubwa ikiwa ni ukosefu wa ujuzi jambo ambalo linaweza kusababisha migogoro mikubwa katika nchi husika.
Amesema mradi wa dumisha amani unalenga kuwapatia vijana ujuzi ili wapate shghuli za kufanya kwa kuweka mifumo ya kuimarisha amani.
“Vijana wengi bado wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa ajira, kutengwa kijamii na ukosefu wa ujuzi, hali inayoweza kuchochea migogoro na kudhoofisha mshikamano wa kijamii”.
Amesema kupitia mradi wa Dumisha Amani, UNDP kwa kushirikiana na wadau wake imewekeza katika mafunzo ya ufundi stadi kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya vijana, ambapo jumla ya vijana 60 Zanzibar walipatiwa mafunzo hayo, wakiwemo vijana 30 kutoka Unguja na 30 kutoka Pemba, waliochaguliwa kati ya waombaji 170.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Ali Haji, amesema vijana waliopata mafunzo hayo sasa wako tayari kuingia katika soko la ajira kutokana na ujuzi walioupata.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake waliohitimu mafunzo hayo, Simni Ali Kwanza amesema wamejifunza kwa vitendo hatua ambayo imewajengea sio tu uwezo, bali pia kujiamini hivyo kwasasa wanaweza kufanya kazi katika mazingira yoyote.
“Awali tulijifunza kwa nadharia pekee, lakini sasa tumepata ujuzi wa vitendo utakaotuwezesha kuajiriwa au kujiajiri wenyewe na kujinasua na changamoto za kiuchumi,” amesema Simni
Azimio la vijana Amani na Usalama 2250 limebainisha maeneo makuu matano ambayo nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wanapaswa kutekeleza, maeneo hayo ikiwa ni ushiriki, ulinzi, uzuiaji, ushirikiano uondoshaji na urejeshaji.
Wanaharakati, Asasi za kiraia na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa waliungana katika kutambuliwa nafasi ya kijana katika mchakato wa kujenga amani na usalama duniani kwasababu vijana wamekuwa waathirika wakuu katika migogoro na vita duniani.
Kutokana na huo, Agosti 22, 2015 katika mji wa Amman, Jordan walikuja na tamko la vijana, amani na usalama ambalo liliweka msingi azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la vijana Amani na Usalama 2250.