LHRC WATOA TAMKO LA HALI YA HAKI ZA BINADAMU TANZANIA

Wakili Fulgence Massawe Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho LHRC
 :::::::::

 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa tamko kwa vyombo vya habari kikieleza hali ya haki za binadamu nchini, miezi miwili baada ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu iliyoadhimishwa Desemba 10, 2025.

Kituo hicho kimeeleza kuwa bado kuna changamoto kubwa zinazokwamisha ulinzi na utekelezaji wa haki za binadamu katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Akizungumza na Waandishi wa habari mapema Leo jijini Dar es salaam , Wakili Fulgence Massawe ambaye ni Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho LHRC amesema matukio ya ukamataji usiofuata taratibu za kisheria yanaendelea kuripotiwa, hali inayochochea hofu na taharuki miongoni mwa wananchi.

Imebainishwa kuwa katika baadhi ya matukio, askari wanashindwa kujitambulisha wakati wa ukamataji, huku wahusika wakikosa taarifa za msingi kuhusu sababu za kukamatwa kwao.

LHRC pia imeeleza kuwa baadhi ya watuhumiwa wanashikiliwa kwa muda mrefu bila kufikishwa mahakamani au kunyimwa dhamana, hata kwa makosa yenye dhamana kisheria.

Hali hiyo, kwa mujibu wa kituo hicho, inasababisha kuporomoka kwa imani ya wananchi kwa vyombo vya dola na taasisi za haki jinai.

Katika tamko hilo, LHRC imeonya dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka yanayofanywa na baadhi ya viongozi wa kisiasa, hasa kuingilia masuala ya jinai yanayopaswa kushughulikiwa na vyombo vya kisheria.

Imeelezwa kuwa vitendo hivyo vinakiuka misingi ya utawala wa sheria na kuhatarisha haki za msingi za wananchi.

Aidha, kituo hicho kimesikitishwa na kuendelea kuripotiwa kwa matukio ya watu kutekwa au kupotezwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

LHRC imesema matukio hayo yanakiuka haki ya kuishi na usalama wa mtu, na yanahitaji uchunguzi wa haraka, wa kina na wa uwazi ili kubaini wahusika na kutoa majibu kwa jamii.

Kutokana na hali hiyo, LHRC imezitaka mamlaka husika kutoa taarifa kwa wakati pale mtu anapokamatwa, kuhakikisha taratibu za kisheria zinafuatwa, na kuwapa dhamana au kuwaachia huru wote wanaoshikiliwa kwa makosa yenye dhamana.

Kituo hicho kimesisitiza kuwa hatua hizo ni muhimu katika kulinda haki, usalama na imani ya wananchi kwa mifumo ya utawala wa sheria nchini.