Dar es Salaam. Miaka miwili imetimia tangu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alipofariki dunia, akiacha kumbukumbu ya uongozi uliotukuka na mfano wa kuigwa kwa viongozi vijana wa sasa.
Lowassa alifariki dunia Februari 10, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu kwa maradhi ya shinikizo la damu, matatizo ya mapafu na kujikunja kwa utumbo.
Makamu wa Rais wa wakati huo, Dk Philip Mpango, akiwa kwenye ziara yake wilayani Longido, Arusha kabla ya kuiahirisha, alitangaza kutokea kwa kifo cha kiongozi huyo na kutangaza siku tano za maombolezo ya kitaifa huku bendera zikipepea nusu mlingoni.
Siku hii ni kumbukumbu ya pekee kwa mwanasiasa huyo anayetajwa na makundi tofauti ya watu kama kiongozi aliyejali utu, aliyependa kuona matokeo, aliyeuchukia umaskini na aliyependa uwajibikaji kuanzia kwake binafsi na watu wengine.
Aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli enzi za uhai wake akifurahia jambo Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa wakati akirejea CCM kutoka Chadema katika hafla iliyofanyika kwenye ofisi ndogo za CCM, Dar es Salaam. Picha na Mtandao
Akiwa Waziri Mkuu, Lowassa alijijengea umaarufu kwa kusimamia ujenzi wa shule za kata nchi nzima, sera ya Serikali ya awamu ya nne, aliyoibeba kwa dhati na kuhakikisha inafanikiwa kwa kila kata nchini kuwa na shule ya sekondari.
Vilevile, alisimamia ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), akiibana mifuko ya hifadhi za jamii nchini kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa chuo hicho kikubwa nchini kikiwa na uwezo wa kupokea wanafunzi 40,000.
Akiwa mgombea urais kupitia Chadema, Lowassa alichagiza umuhimu wa kufanya mabadiliko, akiibeba ajenda hiyo kama ahadi yake kwa wananchi. Mikutano yake ya kampeni ilipewa jina la “mafuriko” kutokana na wingi wa watu waliojitokeza kumsikiliza.
Marafiki, wasaidizi, wanasiasa na wote aliowahi kufanya nao kazi, wanamwelezea Lowassa kama kiongozi aliyejitoa kuwatumikia wananchi na kuhakikisha mipango yote ya Serikali inatekelezwa kikamilifu.
Kwenye ulingo wa siasa, wanamwelezea kama mwanasiasa aliyejali utu na ustaarabu kwa kuwa, hakutukana watu wala kuwadhalilisha anapokuwa jukwaani, hasa wale alioshindana nao katika kuwania nafasi ya uongozi, iwe ubunge au urais.
Licha ya kuwa kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa muda mrefu katika maisha yake, Lowassa aliwahi pia kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kupata nafasi ya kugombea urais mwaka 2015, kabla ya kurudi tena CCM.
Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa wakati akitambulishwa kwa mara ya kwanza katika Kamati Kuu ya Chadema walipokutana Bahari Beach Kunduchi jijini Dar es salaam. Picha na Maktaba
Watu mbalimbali waliokuwa naye karibu wamemwelezea kwa namna walivyomfahamu huku wakieleza sifa yake kuu ya uchapakazi, ustahimilivu na kuheshimu mawazo ya wengine, sifa ambazo viongozi wengi hawana.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Februari 10, 2026 msaidizi wake wa karibu, Abubakar Liongo amesema Lowassa alikuwa na mapenzi ya dhati kwa Taifa lake na aliendesha siasa kwa uungwana mkubwa kwa kuwa, alipokuwa jukwaani, hakuwahi kutukana mtu.
“Alikuwa ni binadamu wa kiwango cha juu sana, ndiyo maana mawimbi ya siasa zake bado yanavuma. Alikuwa ni kiongozi mvumilivu, mstahimilivu…alipenda zaidi kujadiliana, kuvumiliana na alikuwa msikivu, anakupa sikio lake,” amesema Liongo.
Pia, amesema wanapomkumbuka Lowassa, wanakumbuka mbuyu wa siasa na uongozi wenye matawi yaliyotawanyika kila mahali, uliyoanguka lakini kivuli chake bado kipo.
Rais Samia Suluhu Hassan akiweka shada la maua katika kaburi la Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa. Picha na Maktaba
“Mawimbi yake ya siasa bado yanaendelea kuvuma na kwa hakika yatazidi kuendelea kuvuma. Tunakumbuka utu, unyenyekevu, uungwana, upendo, uchapakazi wenye maono na mapenzi ya dhati kwa taifa lake,” amesema.
Pia, amesisitiza kwamba, wanamkumbuka kama kiongozi wa vitendo, aliyetaka matokeo chanya kwa haraka.
Amesema ameacha alama kubwa zikiwamo ujenzi wa shule za kata nchi nzima pamoja na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Mwanasiasa mkongwe nchini, Paul Kimiti amemwelezea Lowassa kama kiongozi aliyekuwa na msimamo na kwamba akitaka jambo lake litakuwa na siyo ‘blahblah’ za kuwahadaa wananchi kwa maneno matupu.
“Nimefanya naye kazi, nilikuwa naye Wizara ya Kilimo na Mifugo baadaye tukatenganishwa, Lowassa alikuwa mtu mwenye msimamo, akiamua jambo hapigi maneno,” amesema Kimiti.
Pia, amesisitiza kwamba Lowassa alikuwa kiongozi anayependa matokeo yaonekane kwa ajili ya kuwasaidia wananchi na alikuwa mfano mzuri wa viongozi wanaopenda mafanikio na mabadiliko kwenye maisha ya wananchi.
Mwanasiasa mkongwe nchini, Paul Kimiti. Picha na Mtandao
Kimiti ambaye ni mtaalamu wa kilimo na mifugo, amesema walishirikiana zaidi na Lowassa hata baada ya kutenganishwa wizara na utekelezaji wake wa mambo ulikuwa thabiti kutokana na utendaji wake.
Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga amesema Lowassa alitengenezwa kuwa kada mzuri wa CCM na Serikali.
“Chama cha Mapinduzi kilimtafuta, kilimuona ni kijana mzuri na ana uwezo na anaweza kuandaliwa kuja kuongoza Watanzania wenzake; na kweli chama kilifanikiwa kumchagua mtu aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kuendesha shughuli za chama na Serikali,” amesema.
Kanali Lubinga amesema Lowasa alifanya kazi vizuri kuanzia akiwa mtendaji ndani ya CCM Idara ya Oganaizesheni na aliteliuwa kuwa Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).
Baada ya kuhudumu AICC, Kanali Lubinga amesema Lowassa alikwenda kugombea ubunge na kushinda, kisha kupewa wizara, ofisi ya Waziri Mkuu na kutokana na utendaji wake, akauteliwa kuwa Waziri wa Ardhi.
Kanali Lubinga amesema Lowassa alikwenda kugombea urais japo hakupata na kuendelea na shughuli zingine.
Amesema lengo la Lowassa kugombea nafasi hiyo ilikuwa kuwasaidia Watanzania kuwaletea maendeleo.
“Ametimiza wajibu wake kama kada wa CCM, wizara zote alizopita na idara za chama, amefanya kazi vizuri,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Amani Golugwa amesema mchango wa Lowassa katika siasa za mageuzi nchini umeacha kumbukizi na alama kubwa.
Golugwa amesema kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2015, akiwa mgombea urais kupitia Chadema, Lowassa alibeba ajenda ya mabadiliko ambayo bado ni hitaji la Watanzania wa sasa.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Amani Golugwa. Picha na Mtandao
Amesema mabadiliko ambayo Chadema ilianza kuyahubiri tangu mwaka 2015, yalikuwa yamejikita katika uchumi, huduma za Serikali kwa jamii, huduma zisizo na urasimu na mabadiliko ya kupiga vita umaskini.
“Lowassa alizungumzia jambo kubwa ambalo matokeo yake tunayaona leo, suala la ajira kwa vijana. Alisema hili janga la kutotoa ajira au kutengeneza mazingira ya vijana kujiajiri ni bomu litakalolipuka baada ya muda,” amesema.
Golugwa amesema miaka 10 baada ya uchaguzi 2015, kauli hiyo inaonekana lakini pia hitaji la mabadiliko ya Katiba, sheria za kutoa haki, mifumo ya utawala bora, agenda iliyobebwa na mgombea wao huyo wa nafasi ya urais, bado hadi sasa ina mantiki.
“Mchango wa Lowassa kwenye siasa za ushindani umeweka alama kubwa sana, leo Chadema tunajivunia historia ya kuwa na maisha tukiwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Lowassa aliyetoka chama tawala na kuhamia upinzani na kuibeba ajenda ambayo ilikuwa ina mantiki kwa Taifa wakati huo na hata sasa,” amesema.
Amesema ni bahati mbaya mchango huo wa Lowassa hausemwi kwa kina licha ya kuwa na mchango mkubwa katika siasa za upinzani.
Aliyekuwa mgombea mwenza wa urais wa Tanzania kupitia Chadema, mwaka 2015, Juma Duni Haji amesema jambo analolikumbuka kwa Lowassa ni namna alivyowajibishwa kwa kesi ya ufisadi wa Richmond.
“Waziri Mkuu wa wakati ule (Lowassa) hawezi kufanya uamuzi wowote bila uamuzi wa Baraza la Mawaziri au Rais na alisimama bungeni akasema ‘shida yenu uwaziri mkuu, basi nauachia.’ Hiyo ni sifa ya mtu mwaminifu, hang’ang’anii kitu ambacho sio chako, kama mtu anakuona tatizo basi unaondoka,” amesema.
Babu Duni ambaye kwa sasa ni mwenyekiti mstaafu wa ACT Wazalendo, amesema sifa hiyo ya Lowassa imekuwa sifa yake, hawezi kulazimisha vitu kama watu wameona ni tatizo basi anawajibika.
Aliyekuwa mgombea mwenza wa urais wa Tanzania kupitia Chadema, mwaka 2015, Juma Duni Haji. Picha na Mtandao
Amesema akiwa mgombea mwenza wa urais, amefanya kazi na Lowassa na alikuwa akimheshimu na kumsaidia kwa namna zote wakati wa kampeni za uchaguzi.
Amesema kuwa uchaguzi wa mwaka 2015 waliibuka washindi lakini ilishindikana kuongoza Serikali kutokana na mifumo ilivyo.
Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 katika Kijiji cha Ngarash, Monduli na ndiye mtoto mkubwa wa kiume kwa Mzee Ngoyai Lowassa.
Alianza kusoma katika Shule ya Msingi Monduli kati ya mwaka 1961–1967. Kisha akaendelea kwenye Shule ya Sekondari Arusha kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne kati ya mwaka 1968 – 1971, kabla ya kumalizia kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Milambo mkoani Tabora mwaka 1972–1973.
Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa akifurahia jambo na swahiba wake wa miaka nyingi na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete. Picha na Mtandao
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1974–1977 na kuhitimu Shahada ya Sanaa katika Elimu na baadaye Chuo Kikuu cha Bath, Uingereza kwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Maendeleo (mwaka 1983–1984).
Baada ya kumaliza chuo kikuu, Lowassa alifanya kazi ndani ya CCM akiwa ofisa wa ngazi ya juu kuanzia wilaya, mkoa na baadaye makao makuu kati ya mwaka 1977–1989.
Aliajiriwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC), mwaka 1989–1990.
Lowassa alimuoa Regina na wana watoto watano, wasichana wawili na wavulana watatu. Watoto hao ni Fredrick, Pamella, Adda, Robert na Richard.