KIPA wa Dodoma Jiji, Ally Salim amepata majeraha yatakayomuweka nje ya uwanja kwa takribani mwezi mmoja.
Salim aliye na clean sheet tano akishika nafasi ya pili nyuma ya Erick Johola wa Mashujaa mwenye sita, aliumia bega katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City, iliyopigwa Uwanja wa Sokoine, Feb 3, 2026.
Akizungumza na Mwanaspoti, Salim alitaja sababu ya jeraha hilo kuwa ilipigwa krosi wakati anakwenda kuokoa mpira alikutana na mchezaji aliyekuwa anataka kuupiga kwa kichwa kilichofikia begani kwake na kwa mujibu wa daktari alimtaka apumzike kwa mwezi mmoja ili apate matibabu.
“Naendelea na matibabu, nipo nyumbani kujiangalizia hali yangu na kuzingatia ninachoelekezwa na daktari ili niweze kupona kwa uharaka kwani napata na muda mzuri wa kupumzika,” amesema Salim na kuongeza;
“Ingawa kwa sasa maumivu yamepungua kidogo tofauti na mwanzo, naamini nitakaa sawa na kurejea katika majukumu yangu ya uwanjani.”
Ukiachana na majeraha, amesema msimu huu kwake ni wa tofauti, kutokana na kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara, kitu kinachorejesha kiwango bora na kujiamini.
“Mchezaji asipocheza inakuwa ngumu kuonyesha kiwango chake kwani kadri anavyocheza ndivyo anakuwa bora, ndiyo maana niliona ni msimu ulioanza vizuri kwa upande wangu, ingawa kwa sasa nina majeraha ya bega,” amesema Salim anayemiliki ‘clean-sheets’ tano.