NAIBU WAZIRI LONDO AITAKA FCC KUIMARISHA USHINDANI NA KULINDA MASOKO YA NDANI

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Dennis Londo akizungumza na wafanyakazi wa FCC wakati alipotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kujua majukumu ,jijini Dar es Salaam.

************

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, ameielekeza Tume ya Ushindani (FCC) kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ndani, kukuza mauzo ya nje na kufanya kazi kwa tija ili kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Londo aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipofanya ziara katika Tume hiyo, akisisitiza umuhimu wa kulinda masoko ya ndani, kuvutia wawekezaji wa nje na kuhakikisha mitaji inalindwa huku faida zikiongezeka.

Amesema FCC ina jukumu muhimu la kusimamia ushindani wa haki katika soko ili kujenga imani ya walaji, akibainisha kuwa sekta ya huduma ndiyo sehemu ambayo wananchi hukutana moja kwa moja na Serikali.

Kwa mujibu wa Londo, ushindani wenye uwazi husaidia walaji kupata bidhaa na huduma bora, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi kwa ujumla.

Aidha, amesema ni dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona FCC inaendelea kulinda ushindani kwa kufuata sheria na taratibu, huku walaji wakipewa nafasi ya kutoa taarifa sahihi kuhusu huduma wanazozipata.

Ameongeza kuwa FCC inapaswa kuendelea kutoa huduma bora zitakazochochea uwekezaji wa viwanda, kuongeza ajira kwa vijana na kulinda ubora wa bidhaa za ndani ili Tanzania iendelee kunufaika na biashara ya kimataifa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema Tume imejipanga kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na wadau wengine kuhakikisha ushindani wa haki, ulinzi wa mlaji na udhibiti wa bidhaa bandia vinaimarishwa kwa maendeleo ya uchumi jumuishi.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Dennis Londo akizungumza na wafanyakazi wa FCC wakati alipotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kujua majukumu ,jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa FCC Dkt.Aggrey Mlimuka akizungumza kuhusiana na majukumu yao kuishauri Taasisi yao katika utoaji huduma ,jijini Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu FCC Khadija Ngasongwa akitoa maelezo kuhusisiana na Majukumu ya Taasisi hiyo kwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara  Dennis Londo wakati alipotembelea Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Wafanyakazi  wakimsikiliza Naibu Waziri wakati alipotembelea ofisi hiyo jijini Dar es Salaam. 

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Dennis Londo akiwa katika picha ya pamoja na makundi ya muundo wa FCC ,jijini Dar es Salaam.