Pingamizi madai wakili kutokuwa na leseni yazua mvutano, Mahakama kutoa uamuzi kesho

Unguja. Hoja ya madai ya wakili aliyesaini hati za maombi ya yaliyofunguliwa na wagombea 17 wa ACT Wazalendo Mahakama Kuu ya Zanzibar kuzuia uteketezaji wa baadhi ya nyaraka za uchaguzi imesababisha mahakama hiyo kuahirisha kesi hiyo mpaka kujiridhisha na madai hayo.

Maombi madogo ya madai namba 18 ya mwaka 2026 yalifunguliwa Ijumaa Februari 6, 2026 chini ya hati ya dharura.

Hatua hiyo imefikiwa leo Februari 10, 2026 Mahakama Kuu Tunguu wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo baada ya upande wa Jamhuri kuweka pingamizi kuhusu hati hiyo ukidai aliyeapa licha ya kuwa ni wakili, lakini hana sifa kwa sababu hana leseni ya kamishna wa kiapo.

Akifafanua kuhusu hilo, wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Said Salim Said amedai watawasilisha pingamizi tano chini ya kifungu namba 129 sura ya nane ya sheria za Zanzibar.

Amesema katika kifungu cha 38 (1) kimeeleza wazi kwamba ni kosa mawakili kujitambulisha mtaalamu wa sheria bila kuwa na leseni.

“Kwa msingi huo, hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani imeapiwa na wakili Ussi Khamis Haji Februari 5, 2026 kama yeye ni kamishna wa kiapo, akaweka tarehe na kusaini akijua hana leseni.

“Unaweza kuwa wakili lakini usiwe kamishna wa viapo, tofauti na Tanzania Bara ambapo mtu anaweza kuwa wakili moja kwa moja anakuwa kamishna lakini sisi (Zanzibar) sheria ipo wazi sana,” amedai.

Amedai leseni ya viapo inaisha kila mwaka ambapo wakili husika anatakiwa kuilipia kila mwaka, lakini kwa taarifa ambazo wamezipata wakili huyo inaonekana hana leseni kwa mwaka jana hadi mwaka huu hajapata.

Katika kuthibitisha hilo, wakili Said ametaka kuwasilisha barua waliyoipata leo Februari 10, 2026 kutoka ofisi ya Mrajisi wa Mahakama ikithibitisha wakili huyo kutokuwa na leseni.

Hata hivyo, aliwekewa pingamizi na wakili wa upande wa waleta maombi, Rajab Abdalla Rajab akidai barua hiyo inatakiwa itoke kwa ushahidi na aliyeiwasilisha anatakiwa aulizwe kuhusu barua hiyo, lakini kwa msingi wa hatua lililopo shauri hilo hakuna uwezekano huo.

Pia, amesema barua hiyo inatakiwa iwasilishwe wakati wa kutoa ushahidi na sio wakati huu wa usikilizaji wa maombi.

“Mheshimiwa Jaji hii barua inatakiwa itoke kwa ushahidi na ina process zake (taratibu, hatua zinazofuatwa), lazima tufanye Cross Examination (mahojiano ya upande wa pili), inabidi mahakama itupe nafasi tumuhoji, halafu yeye sio shahidi kwa hiyo wangeleta maombi maalumu kuiwasilisha barua hii, kwa hiyo tunaomba barua isipokewe,” amedai.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji anayesikiliza shauri hilo, Salma Hassan, aliahirisha shauri hilo kwa muda, mahakama iliporejea akasema uamuzi wake, hatapokea barua hiyo.

Hatua hiyo ikatoa fursa ya wakili wa Serikali, Said kuendelea kueleza zaidi kuhusu kwa nini wakili huyo hana sifa za kusaini viapo hivyo.

Wakati akiendelea, amesimama wakili wa waleta maombi, Rajab akasema hakuna sababu ya kupoteza muda wa mahakama akashauri mahakama ijiridhishe ikiwa kama ni kweli wakili huyo hana sifa au vinginevyo na itoe uamuzi leo.

Hata hivyo, licha ya Jaji kukubaliana na hoja hiyo ya kujiridhisha na kwamba ana uwezo wa kupata majibu leo lakini anatakiwa apate muda wa kuandika uamuzi huo, hivyo ameahirisha shauri hilo hadi Ijumaa Februari 13, 2026 atakapotoa uamuzi na kusikiliza maombi hayo.

Katika shauri hilo upande wa waleta maombi umewakilishwa na mawakili wawili, Rajab Abdalla Rajab na Suleiman Abdalla huku upande wa wajibu maombi ukiwakilishwa na mawakili wanne: Said Salim Said kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Maulid Ame Mohamed kutoka ZEC, Mbarouk Suleiman Othman na Ali Issa Abdalla.

Chimbuko la shauri waombaji ambao ni wadai katika mashauri ya uchaguzi namba mbili hadi 18 za mwaka 2025, waliwasilisha maombi hayo chini ya hati ya dharura.

Hatua hiyo ilikuja kufuatia tangazo la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa umma likielezea nia ya kuteketeza nyaraka zote za uchaguzi wa mwaka 2025.

Maombi hayo yanataka nyaraka zote za uchaguzi zibaki kama zilivyo hadi hapo maombi hayo yatakaposikilizwa kwa pande zote mbili.

Nyaraka ambazo waombaji wameomba zizuiwe kuharibiwa ni fomu PS namba tisa fomu ya makabidhiano ya orodha ya vifaa  zilizojazwa na wasimamizi wa vituo vyote vya kupigia kura vya Jimbo la Pangawe, Malindi, Kiembe Samaki, Chumbuni, Chaani, Makunduchi, Mwera, Nungwi, Tumbatu, Mkwajuni, Bumbwini, Mpendae, Mtoni, Welezo, Amani, Mwanakwerekwe na Kijini kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Nyingine ni fomu PS namba 13B hesabu ya karatasi za kura, fomu namba 16 fomu ya kufunga kituo cha kupiga kura na fomu PS namba 17B ya matokeo, fomu MWJ namba 19B ya majumuisho ya kura na orodha ya wapiga kura ya mapema wa majimbo hayo.