Geita. Serikali mkoani Geita imesema haitambui uwepo wa mwekezaji yeyote mwenye mkataba halali katika eneo la Kitongoji cha Katoro Senta, Kata ya Katoro, Mji Mdogo wa Katoro wilayani Geita.
Kauli hiyo imetolewa kufuatia sakata la madai ya uwekezaji katika eneo hilo, lililoambatana na mvutano mkali uliogeuka vurugu kati ya Mbunge wa Geita, Joseph Kasheku ‘Musukuma’, na mtu aliyetajwa kuwa mwekezaji, Rashid Kwanzibwa.
Tukio hilo liliibua maswali kuhusu uhalali wa umiliki wa ardhi, taratibu za uwekezaji na uwajibikaji wa taasisi husika katika kusimamia mali ya umma.
Uamuzi huo umetolewa leo Februari 10, 2026, na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, wakati akiwasilisha matokeo ya uchunguzi wa tume iliyoundwa chini ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kufuatilia mgogoro wa ardhi kati ya Kamati ya Uchumi na Fedha ya Halmashauri ya Manispaa ya Geita na Rashid Kwanzibwa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Shigela amesema uchunguzi wa Serikali umebaini kuwa hadi sasa hakuna mtu anayetambulika rasmi kama mwekezaji katika eneo hilo wala hakuna mkataba wowote wa uwekezaji uliosainiwa kisheria.
“Kwa sasa tunavyozungumza, timu yetu imebaini mpaka sasa hakuna mtu anayeitwa mwekezaji wala hakuna mkataba uliosainiwa katika eneo hili. Hivyo, kama kuna mtu anayejiita mwekezaji, hana mkataba wala hajakabidhiwa eneo kwa shughuli za uwekezaji,” amesema Shigela.
Amefafanua kuwa mwaka 2018, Serikali kupitia Idara ya Ardhi ilifanya zoezi la upimaji wa eneo la uwanja wa michezo uliopo Katoro na kuliweka rasmi chini ya umiliki wa chama cha CCM.
Hata hivyo, maeneo yanayozunguka uwanja huo, yakiwemo ofisi za kata na tarafa, ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Katoro, ghala la kijiji, mahakama ya mwanzo na ofisi za ardhi, hayakupimwa kutokana na zoezi hilo kusimama kabla ya kukamilika.
Kutokana na hali hiyo, Shigela amemuagiza Kamishina Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Geita, kwa kushirikiana na wataalamu wa ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, kuendelea na mchakato wa upimaji, upangaji na umilikishaji wa maeneo yote yaliyosalia ili kuondoa utata unaoweza kujitokeza siku zijazo.
Amesisitiza kuwa zoezi hilo litakuwa shirikishi na kuwahusisha wadau wote muhimu.
Kuhusu hatima ya Rashid Kwanzibwa, Shigela amesema suala hilo sasa liko mikononi mwa CCM, ambao ni wamiliki halali wa eneo la uwanja wa michezo.
Ameeleza kuwa chama hicho tayari kimeanza mchakato wa ndani kupitia vikao vyake kuanzia ngazi ya tawi, kujadili aina ya mradi unaofaa kuanzishwa, tija yake kwa wananchi wa Katoro na manufaa kwa chama, kabla ya kumpata mwekezaji atakayekidhi vigezo.
Aidha, Shigela amesema Serikali na CCM kwa pamoja zitatambua umuhimu wa sekta ya michezo, hivyo uwekezaji wowote utakaoruhusiwa hautapaswa kuathiri uwepo na matumizi ya uwanja wa michezo, ambao pia umekuwa ukitumika kwa shughuli za kijamii.
Mmoja wa wakazi wa Katoro, Francis Nganyila, amesema ameridhishwa na msimamo wa Serikali, lakini ameshauri kuwepo uwazi zaidi na ushirikishwaji wa wananchi pale maeneo yanapohamishwa kutoka umiliki wa serikali za mitaa kwenda kwa vyama vya siasa.
Sakata hilo lilianza Januari 23, 2026, baada ya kusambaa mitandaoni picha na video zikionyesha Kamati ya Uchumi na Fedha ya Halmashauri ya Manispaa ya Geita ikimsimamisha Kwanzibwa kuendelea na ujenzi kwa madai ya kutofuata taratibu.
Baadaye, mvutano huo uliibuka wazi na kuhusisha kurushiana maneno na ngumi kati ya Kwanzibwa na Mbunge Musukuma, pamoja na Mbunge wa Katoro, Kija Ntemi.
Kufuatia tukio hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, alitoa siku 14 kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kufanya uchunguzi wa kina, huku Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Leonard Akwilapo, akituma wataalamu kuungana na wenzao wa TAMISEMI kuhakikisha mgogoro huo unapata ufumbuzi wa kitaalamu.