Serikali yataka tafiti zenye kusaidia maendeleo ya uchumi wa Taifa

Arusha. Serikali imewataka wahitimu wa masomo ya kifedha kuwekeza nguvu zao zaidi katika kufanya tafiti zinazolenga kutatua changamoto zinazochochea ukuaji wa uchumi wa Taifa, kuboresha usimamizi wa fedha za umma, kuunda ajira, kuendeleza ubunifu, na kutumia teknolojia kwa ufanisi.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Omar Mussa, wakati wa mahafali ya 27 (Duru ya Pili) ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), iliyohitimisha safari ya masomo ambapo jumla ya wahitimu 2,250 walipatiwa shahada za uzamili.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri, Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula amesema kuwa Tanzania inahitaji wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu katika usimamizi wa fedha za umma, tathmini ya miradi ya maendeleo, udhibiti wa matumizi, na mapambano dhidi ya ubadhirifu.

“Mnahitimu katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto za kiuchumi, maendeleo ya teknolojia, na ushindani mkali, hivyo tunahitaji wataalamu wabunifu, waadilifu, na waliojiwekea kujifunza muda wote namna ya kusaidia kupambana na mdodoro wa uchumi wa dunia na kufikia malengo yetu ya Taifa ,” amesema Luswetula.

Ametumia nafasi hiyo kuwataka wahitimu kuhakikisha tafiti zao zinashughulikia changamoto halisi, zikihusisha kuimarisha mifumo ya fedha za umma, kukuza ukuaji wa uchumi unaojumuisha jamii zote, kuongeza fursa za ajira, kuendeleza ubunifu na kutumia teknolojia kwa uwajibikaji.

Aidha, Luswetula ameongeza kuwa sekta kama fedha, uhasibu, uchumi, benki, biashara, usimamizi wa miradi, ununuzi, rasilimali watu, uongozi na utawala ni muhimu katika kuhakikisha rasilimali za Taifa zinatumika kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji.

Mkuu wa IAA, Profesa Eliamani Sedoyeka, amesema kuwa jumla ya wahitimu 2,250 wamehitimu wakiwemo wanaume 1,369 na wanawake 881.

Amesema kundi hilo wamehitimu katika programu zilizoundwa kuandaa viongozi, wataalamu, na wasomi watakaochangia agenda ya maendeleo ya Tanzania.

Profesa Sedoyeka pia amesema kuwa mfumo wa ujifunzaji wa IAA unaochanganya masomo ya ana kwa ana na mtandaoni umewawezesha wataalamu kuendelea na masomo bila kuathiri majukumu yao ya kazi au huduma kwa jamii.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya IAA, Dk Mwamini Tulli, amesema chuo kinawekeza katika wataalamu wake kwa kuwasaidia kusomea shahada za uzamivu (PhD) ndani na nje ya nchi.

“Kwa mwaka wa masomo 2025/2026, wahadhiri 115 wameandikishwa katika programu za PhD ndani na nje ya nchi.”

Dk Tulli amewataka wanafunzi kuhakikisha tafiti zao zinatumika kuboresha sera, mifumo, na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Pia amesema kwa sasa wanajiandaa kufungua kampasi mpya Bukombe mkoani Geita, ikitanguliwa na za Arusha, Babati, Bukombe, Dar es Salaam, Dodoma, na Songea.

“Aidha, idadi ya wanafunzi imeongezeka hadi 22,936 mwaka huu wa masomo, kutoka 21,309 mwaka uliopita, na kuashiria ongezeko zaidi baada ya usajili wa shahada ya uzamili unaotarajiwa kufanyika Machi mwaka huu” amesema.