Sh120 bilioni kuifufua Mutex | Mwananchi

Musoma. Zaidi ya Sh120 bilioni zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kufufua uzalishaji wa kiwanda cha nguo cha Mutex kilichopo mjini Musoma baada ya kiwanda hicho kuacha kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

Kiasi hicho cha fedha kinatarajiwa kutumiwa na mwekezaji ambaye hata hivyo hajawekwa wazi huku ikielezwa kuwa hivi sasa Serikali iko katika taratibu za mwisho za makubaliano na mwekezaji huyo.

Taarifa hiyo imetolewa mjini Musoma Jumanne Februari 10,2026 na Mbunge wa Musoma Mjini, Mgore Miraji alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli zake kwa muda wa siku 100 tangu alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Mgore amesema hadi kufika Juni mwaka huu mwekezaji huyo tayari atakuwa amekabidhiwa eneo la uwekezaji ili aendelee na taratibu zingine, huku akisema kufufuliwa kwa kiwanda hicho kwa namna moja ama nyingine kutachochea kuimarisha uchumi wa mji wa Musoma na watu wake.

“Niliahidi mambo mengi sana lakini kubwa kuliko ni suala la uchumi wa mtu mmojammoja na jimbo kwa ujumla, hili la Mutex ni miongoni mwa mambo niliyoyaahidi nikijua kuwa kiwanda kikifufuliwa watu wa Musoma hususan vijana watapata ajira za moja kwa moja na mbadala, lakini Serikali pia itakuwa na chanzo kingine cha uhakika cha mapato,” amesema

Amesema tayari amewasilisha ombi serikalini ili mwekezaji huyo apewa ekari 11.7 kati ya 25 za kiwanda hicho ili eneo lingine linalobakia litumike kwa ajili ya viwanda vidogovidogo.

“Nasisitiza lengo langu ni kutaka kuona Musoma inakuwa kiuchumi, wananchi wanapata ajira wanakuwa na uhakika wa kupata pesa kupitia fursa mbalimbali zilizopo,” amesema.

Amesema kuwa katika kipindi hicho cha siku 100 pia ametumia zaidi ya Sh53 milioni kwa ajili ya kuwawezesha vijana katika sekta ya elimu na michezo ili waweze kutimiza ndoto zao.

Amesema kati ya fedha hizo, Sh11 milioni zimetumika  kuwalipia ada na mahitaji mengine vijana 50 ambao hivi sasa wameanza mafunzo katika chuo cha ufundi stadi (Veta) kilichopo Musoma.

Pia Sh28.9 milioni zimetumika kununua mahitaji ya wanafunzi kutoka kaya maskini kwa ajili ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza katika shule mbalimbali jimboni humo.

“Nitoe wito kama bado kuna wanafunzi wana mahitaji hayo ya shule tafadhali tuwasiliane kwani huduma hii bado ipo, tunataka watoto wote waende shule hilo ndilo jukumu lao kwa sasa, hivyo tusikubali vikwazo kama ukosefu wa mahitaji kuwa sababu ya watoto kushindwa kwenda shule,” amesema.

Ameongeza kuwa Sh14 milioni zimetumika kuwapeleka vijana watano kwenye taasisi ya michezo ya Ngasa (Ngasa Academy) iliyopo jijini Dar es salaam kukuza vipaji vyao hasa kwenye mpira wa soka.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema tayari Serikali wilayani humo imeanza uhakika na utambuzi wa kaya zinazostahili kupata bima ya afya kupitia ufadhili wa Serikali.

Amesema kaya 2,834 zinatarajiwa kunufaika na mpango huo wa Serikali ambazo  ni zile zilizopo kwenye mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) katika Manispaa ya Musoma.

“Hadi sasa tumehakiki kaya 811 kazi inayoendelea na ikikamilika tutahamia kwenye makundi mengine ili kuhakikisha kila mtu anafikiwa na mpango huu wa bima ya afya kwa wote, nitoe wito kwa wananchi na wadau wote kushirikiana ili kazi hii ifanyike kwa ufanisi,” amesema

Kuhusu wanafunzi wa kidato cha kwanza Chikoka amesema bado wapo ambao hawajaripoti hadi sasa ingawa hakuweza kutoa takwimu na kwamba msako wa nyumba kwa nyumba unatarajiwa kufanyika ili kujua walipo wanafunzi hao.

“Hali ya uchumi hapa kwa kweli ni mbaya, hakuna mzunguko wa pesa kabisa ili mji uweze kufunguka lazima kuwepo na shughuli nyingi za kiuchumi ambapo viwanda ni miongoni mwa shughuli hizo,” amesema Hemed Chacha.

Chacha amesema ni aibu kwa mji kama wa Musoma kukosa kiwanda hata kimoja hivyo Serikali inatakiwa kufanya haraka kufufua viwanda vilivyokufa mjini Musoma vikiwemo   vya kuchakata samaki.

William Essero amesema kuhusu mpango wa bima ya afya kwa wote uhakiki ufanyike na kuhakikisha wale wanaopata bima kwa gharama za Serikali wawe ni walengwa.

“Wasije wakaanza yale mambo yao ya walengwa wanaachwa halafu wanapewa wale wenye uwezo, haya mambo hatuyataki Serikali ina mipango mizuri sasa watendaji wasiwe kikwazo,”amesema