Sh17 bilioni ‘zitakavyokata kiu’ ya maji Chamwino, kamati yapongeza

Dodoma. Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma imepongeza utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 unaotekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa).

Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Chamwino (DC), Janeth Mayanja imetoa pongezi hizo leo Jumanne, Februari 10, 2026 ilipofanya ziara ya kutembelea mradi huo uliofikia asilimia 68 kujione maendeleo yake.

Mkataba wa mradi huo ulisainiwa Juni 6, 2022 na utekelezaji wake ulianza mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika Agosti 10, 2026, huku mkandarasi amepewa maelekezo na Wizara ya Maji kuhakikisha ifikapo Machi 31, 2026 awe ameanza kufanya majaribio ya mradi.

Mayanja amesema kamati ya siasa imeridhishwa na utekelezaji wa mradi huo ambao utakwenda kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Chamwino, hasa katika maeneo yenye mgao wa maji, ikiwemo Kata ya Chamwino, Msanga na Buigiri.

Amesema, wananchi wa Wilaya ya Chamwino wanamshukuru Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya katika Wilaya ya Chamwino.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Chamwino, George Malima, ameipongeza Wizara ya Maji na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa)kwa kusimamia mradi huo na kuomba mkandarasi kukamilisha kwa wakati mradi huo.

Akisoma taarifa ya mradi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Meneja wa Duwasa, Kanda ya Chamwino, Gray Mbalikila amesema lengo la mradi huo ni kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi katika Mji wa Chamwino, ambapo kukamilika kwake  kutachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja kupunguza magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa maji.

Amesema gharama za mradi huo ni Sh17 bilioni ambazo zinahusisha uchimbaji wa visima virefu vinane ambavyo vimekamilika, ujenzi wa tanki la kuvunia maji la lita 500,000 na miundombinu ya kusukuma na kutibu maji katika eneo la Chamwino.

Kazi nyingine zinazofanyika katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa tanki la lita 200,000 katika eneo la Msanga na uchimbaji na ulazaji wa bomba za kipenyo kikubwa cha inchi sita hadi 16 kwa umbali wa kilomita 47.

Kukamilika kwa mradi huo utaongeza upatikanaji wa majisafi kutoka asilimia 91 ya sasa hadi asilimia 100 na utaenda kuhudumia wananchi zaidi ya 59,085 katika eneo la kihuduma la Duwasa katika Mji wa Chamwino, ambapo kata nne zenye jumla ya vijiji na mitaa saba na vitongoji 48 watanufaika.