Siri kufanikiwa mkakati wa KKK hii hapa

Dar es Salaam. Uzinduzi wa Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali na wanafunzi wa darasa la I na II, uliofanywa hivi karibuni,  na Rais Samia Suluhu Hassan, ni hatua muhimu na ya kihistoria katika safari ya Tanzania ya kuimarisha sekta ya elimu.

Mkakati huu si wa kawaida, bali ni wa aina yake kwa kuwa umejikita katika misingi ya kisayansi, ushahidi wa kitaalamu na uhalisia wa mazingira ya ujifunzaji ya watoto wetu.

Tumeshuhudia kwa mara nyingine Taifa likiweka mkazo mahsusi katika hatua za mwanzo kabisa za ujifunzaji, likitambua kuwa kusoma, kuandika na kuhesabu maarufu kwa kifupi cha KKK ndizo nguzo kuu za elimu yote inayofuata.

Hatua hii inaonyesha dhamira ya dhati ya Serikali kuondokana na hatari ya kuwa taifa la watu wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu ipasavyo, licha ya watoto wengi kuwa shuleni.

Ni siri iliyo wazi kuwa kwa miaka kadhaa, changamoto ya wanafunzi kufika madarasa ya juu bila umahiri wa msingi wa KKK imekuwa ikijitokeza. Wapo wanafunzi wanaomaliza darasa la tatu au la nne bila uwezo wa kusoma kwa ufasaha, kuandika sentensi sahihi au kufanya hesabu za msingi.

Hali hii imekuwa mzigo kwa walimu wa madarasa ya juu na kikwazo kikubwa kwa mafanikio ya elimu kwa ujumla. Mkakati huu unalenga kukata mzizi wa tatizo hilo mapema.

Stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu ndizo msingi wa mafanikio katika ngazi zote za elimu. Mtoto asiyeweza kusoma hawezi kujifunza ipasavyo masomo mengine kama sayansi, historia au jiografia.

Vivyo hivyo, asiye na umahiri wa kuhesabu hushindwa kuelewa hisabati na masomo yanayotegemea takwimu na mantiki. Kwa hali  hiyo, KKK si lengo lenyewe, bali ni daraja la kufikia elimu bora na yenye tija.

Kwa kuzingatia ukweli huo, mkakati uliozinduliwa unaweka mkazo katika elimu ya awali na madarasa ya mwanzo, hatua ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikipewa uzito mdogo ukilinganishwa na elimu ya sekondari au vyuo.

Uamuzi huu unaakisi uelewa wa kisayansi unaoonesha kuwa ubongo wa mtoto hujengeka kwa kasi kubwa katika umri wa awali, na kwamba stadi za msingi hujengeka kwa ufanisi zaidi katika kipindi hicho.

Hata hivyo, pamoja na ubora wa mkakati huu katika maandishi na dhamira njema ya kisera, mafanikio yake yatategemea kwa kiasi kikubwa namna utakavyotekelezwa. Historia ya mipango mizuri kushindwa kuleta matokeo imekuwa ikitufundisha kuwa sera bora bila utekelezaji madhubuti ni sawa na ahadi isiyotimia.

Ili mkakati wa KKK uwe na tija ya kweli, Serikali haina budi kushughulikia kwa umakini masuala kadhaa ya msingi. Kwanza ni uwekezaji wa kifedha. Elimu ya awali na madarasa ya mwanzo inahitaji rasilimali za kutosha, zikiwemo vitabu vinavyolingana na umri wa watoto, vifaa vya kujifunzia, mazingira rafiki ya darasa na miundombinu inayokidhi mahitaji ya watoto wadogo. Bila fedha za kutosha, mkakati huu utabaki kuwa waraka mzuri kwenye makabati.

Pili ni suala la walimu. Walimu wa elimu ya awali na madarasa husika ndiyo uti wa mgongo wa mkakati huu. Hawa ni walimu wanaopaswa kuwa na uelewa wa kina wa saikolojia ya mtoto, mbinu za kisasa za ufundishaji na uwezo wa kutambua changamoto za ujifunzaji mapema. Haiwezekani kutegemea matokeo tofauti wakati walimu hawa hawaandaliwi ipasavyo.

Ni hapa ambapo Serikali inapaswa kubadili mazoea. Mafunzo ya walimu hayawezi kuwa yale ya semina za siku moja au mbili zisizoacha athari ya kudumu. Vivyo hivyo, mfumo wa kumfundisha mwalimu mmoja ambaye baadaye anatarajiwa kuwafundisha wenzake nao nao si wa kisayansi wala wenye ufanisi. Mkakati wa KKK unahitaji walimu wapigwe msasa wa maana, kwa mafunzo endelevu, ya vitendo na yanayoambatana na ufuatiliaji.

Aidha, usomeshaji wa walimu unapaswa kuzingatia ushahidi wa kitaalamu kuhusu namna watoto wanavyojifunza kusoma, kuandika na kuhesabu. Mbinu za kufundisha zisizoendana na sayansi ya ujifunzaji wa watoto zinapaswa kuachwa. Serikali pia ihakikishe walimu wanapatiwa motisha stahiki, ikiwemo mazingira bora ya kazi na maslahi yanayolingana na umuhimu wa kazi wanayoifanya.

Suala jingine muhimu ni ufuatiliaji na tathmini. Mkakati huu unahitaji mfumo madhubuti wa kupima maendeleo ya watoto mara kwa mara ili kubaini mapema wanaochelewa au wenye changamoto maalumu.

Pia, ushiriki wa wazazi na jamii haupaswi kupuuzwa. Elimu ya mtoto haishii darasani pekee. Wazazi wanapaswa kuelimishwa juu ya umuhimu wa KKK na namna wanavyoweza kuchangia, hata kwa njia rahisi kama kusoma na watoto wao nyumbani au kuwahamasisha kufanya mazoezi ya kuhesabu katika shughuli za kila siku.

Kwa ujumla, uzinduzi wa Mkakati wa Kisayansi wa KKK ni ishara njema na uthibitisho wa dhamira ya Rais na serikali yake ya kuwekeza katika rasilimali watu kwa kuanzia kwenye mizizi.

Hata hivyo, mafanikio yake yatapimwa si kwa uzuri wa maneno, bali kwa mabadiliko halisi yatakayoonekana kwa watoto wetu. Tukifanikiwa kujenga umahiri wa KKK kwa watoto wa leo, tutakuwa tumeweka msingi thabiti wa taifa lenye wasomi bora, wabunifu na wenye uwezo wa kushindana katika dunia ya leo na kesho.