………
BIHARAMULO
IMEELEZWA kuwa wananchi wa Kijiji cha Msekwa kata ya Kalenge wilayani Biharamulo mkoani Kagera, wapo mbioni kukimbia Kijiji hicho kutokana na uvamizi wa wanyama pori aina ya viboko ambao wamekuwa wakitishia maisha ya wananchi.
Mbali na hilo, wamedaiwa kuvamia mashamba ya wakulima na kuharibu mazao hali inayotishia kuwepo kwa uhaba mkubwa wa chakula kwa wananchi hao.
Diwani wa kata ya Kalenge, Erick Method, ameeleza hayo kwenye kikao cha robo ya pili ya Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, kilicholenga kujadili hoja mbalimbali za maendeleo ya wilaya hiyo.
“Jambo hili nimekuwa nalieleza hapa mara kwa mara, sasa wananchi wa kijiji cha Msekwa wapo mbioni kukimbia makazi yao kutokana na matishio ya viboko, tuliomba watu wa Tawa na Tanapa wawaondoe wanyama hao lakini utekelezaji wake haupo”.
Diwani wa kata ya Biharamulo mjini, David Mwenenkundwa, amesema siyo busara kwa serikali kufumbia macho malalamiko ya wananchi wa Kijiji cha Msekwa kutokana na matishio ya viboko wanaoharibu mazao ya wakulima.
“Ikumbukwe kuna miongozo ya elimu ya wazazi kupeleka chakula kwaajili ya watoto wao mashuleni, sasa kama viboko wanazidi kumaliza chakula cha wananchi, je ni kipi kitakachopelekwa huko mashuleni”? amehoji Mwenenkundwa.
“Tunataka viboko hao wahame pale na hatupo tayali kuona wananchi wanahama kijiji chao kwa kukimbia wanyama hao, na kama haiwezekani kuwatia basi tuwaruhusu wananchi wenyewe wawale”.
Mbali na mambo mengine, Diwani wa viti maalumu, Ziyuni Hussein, amesema viboko hao pia wamekuwa wakichafua vyanzo vya maji ya wananchi na wananchi kulazimika kunywa maji machafu yasiyofaa kwa matumizi ya binadamu.
Akijibu malalamiko hayo, Kaimu mkuu wa kitengo cha ujirani mwema kutoka Hifadhi ya taifa ya Burigi-Chato, Ayubu Nyakunga, amesema suala la kuwahamisha viboko eneo hilo litachukua muda mrefu kutokana na kuhusisha zaidi ya taasisi moja.
“Kwanza nikiri wazi kuwa suala la viboko limekuwa sugu, na niahidi tu kuanzia kesho tutakwenda eneo hilo ili kuona namna tunavyoweza kuwatisha ili waondoke kwenye makazi ya watu, ila kuwahamisha tunapaswa kuwasiliana kwanza na Tawa pamoja na Tawiri ndo wenye jukumu la kutekeleza hilo” amesema Nyakunga.
Mwisho.


