*******
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga amesema wanamshikilia Bw. Charles Oden Mwakasege (32) fundi simu Mkazi wa Meta Jijini Mbeya na Bw. Isack Charles ‘Bebwa’ mkazi wa Shewa, kwa tuhuma za kuingilia mdumo wa kibiashara wa makampuni ya ukopeshaji wa simu.
Kulingana na Kamanda Kuzaga katika taarifa yake ya leo Jumanne Februari 10, 2026 kwa Vyombo vya habari, watuhumiwa hao walikamatwa katika msako uliofanyika kuanzia Januari 27, 2026 katika maeneo mbalimbali Mkoani humo ambapo watuhumiwa wanadaiwa kubadili simu zilizokopwa na watu mbalimbali kutoka katika makampuni ya ukopeshaji na kuondoa mfumo uliowekwa ili waliokopeshwa wasiweze kufuatiliwa katika kulipa fedha walizokubaliana na makampuni hayo.
“Baada ya watuhumiwa hao kufanyiwa upekuzi kwenye ofisi zao walipatikana wakiwa na simu aina ya Samsung 53, Infinix 21, Tecno 13, Itel 11, Yas 1. Pia walikutwa na vifaa vya kuflash simu ambavyo ni Infinix Box Nongle Cm2 moja, Jtag Adapter Isp 4bit 02, F64 flash ultra box 02, Easy Jtag Plus box 02 Ufi box 01 na Laptop 03.” Amesema Kamanda kuzaga.
Polisi ya Mbeya pia imetangaza kuwashikiliwa watuhumiwa wanne (Wilfred Komba (24), Mwanachuo wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu Iringa, Lenad Shamba (21) mkazi wa Tarime, James Mwakalebela (26) mkazi wa Kyela na Joseph Mkwara (26) kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya Bhangi zikiwa na uzito wa Kilo 45 na gramu 785 katika nyakati tofauti kwenye mabegi, wakidaiwa kuingiza dawa hizo kutoka nchi jirani.
Aidha Kamanda Kuzaga amesema wanawashikilia ndugu wa familia moja ambao ni Solomon Mwambyale (68) na watoto wake wawili, Stephano Mwaisango (32) na Emmanuel Mwaisango (36), kwa tuhuma za mauaji ya Jenti Segelela (87) ambaye alikuwa shemeji yake na mtuhumiwa Solomon, wakidaiwa kumkata na kitu chenye ncha kali kisogoni na kisha kukimbia, chanzo kikiwa ni mgogoro wa mashamba ya ukoo na tamaa ya kujipatia mali kwa njia isiyo halali.
