Dar es Salaam. Wasomi na wataalamu wametakiwa kusimamia ukweli na kutumia taaluma zao kusaidia maamuzi ya viongozi wa kisiasa ili kuisaidia jamii.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, alipozungumza katika baraza la madiwani wa manispaa hiyo lililoketi leo Jumanne Februari 10, 2026.
Katika hotuba yake ya saa mbili, Mapunda amesema wananchi wana imani kubwa na tafiti za wataalamu akiwasihi wasomi kuzitumia, kusaidia kutatua matatizo ya jamii kwa kuwapa maarifa wanasiasa wanaohusika katika kutunga sera na sheria zinazohusu maendeleo ya jamii.
“Wataalamu wasaidieni viongozi, wapeni data na taarifa za kitaalamu ili kusaidia kufanya maamuzi sahihi,” amesema.
Amesisitiza kuwa, wataalamu wanapojitenga na maamuzi ya viongozi wa kisiasa wanaikosesha jamii fursa ya kupata taarifa sahihi na huduma bora zilizojengwa na misingi ya kitafiti na kitaalamu.
“Mlishawahi kuona au kusikia ripoti imepelekwa bungeni ikakwama? Kama hakuna hii inamaanisha wananchi wana imani kubwa na tafiti na mawazo ya wataalamu,” amesema.
Ameeleza kuwa, kukosekana kwa tafiti na mchango wa wataalamu husababisha kukwama kwa miradi, kujengwa chini ya kiwango au kujengwa na kubomolewa hali inayoleta usumbufu kwa wananchi na upotevu wa rasilimali.
“Wataalamu msiwe waoga, hakuna mtu atakayekufukuza kwa kusimamia ukweli wa taaluma zenu maana hata ukiupindisha ukweli haugawanyiki wala hauhitaji kutetewa,” amesema.
“Mradi unajengwa mpaka unakamilika halafu baadaye unakuta mtu anaandika ‘bomoa’ mlikuwa wapi wakati wa mipango mpaka mradi ukafika hapo? Nendeni mkakague haya,” ameelekeza.
Madiwani wakumbushwa aliyewaweka madarakani
Mkuu huyo wa wilaya amewataka madiwani kuwa kazi yao msingi wake ni kuchaguliwa na watu, hivyo wanapaswa kupambana kutekeleza majukumu yao katika kutatua kero za watu.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa hiyo, Jumanne Februari 10, 2026.
Katika baraza hilo lililoketi kwa mara ya kwanza kwa madiwani hao tangu walipoapishwa baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi uliofanyika mwaka jana, Mapunda amesema kwa kuwa nafasi za udiwani zinapatikana kwa kuchaguliwa, kila diwani anatakiwa kukumbuka daima kuwa kilichowaweka madarakani ni kupendwa na watu hivyo wazingatie masilahi ya waliowaweka madarakani.
Akiwapa misingi na miiko ya kuzingatia katika utendaji wao, ameonya kuhusu tabia ya viongozi wa kuchaguliwa wanaojisahau baada na kuacha kuwa karibu na watu katika maeneo yao, akisema hiyo huathiri utendaji wao na hatima yao kisiasa.
“Tusingependa 2030 sura ziwe nyingi mpya, tungependa wengi wenu mrudi, lakini tatizo hapa huwa moja tu, wengi wakichaguliwa hujisahau mapema sana kuwa wanatokana na kuchaguliwa, huwapuuza watu na wao kuja kuwaadhibu uchaguzi unaofuata,” amesema.
Amevitaja vipaumbele vya manispaa hiyo akiwataka madiwani hao kuvibeba kama msingi wa maendeleo ya manispaa hiyo ikiwamo kusimamia tunu za Temeke katika uchumi wa nchi.
“Ndugu madiwani, mjue kuna diwani na kuna diwani wa Temeke, kwani wilaya yetu hii ni tunu muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu maeneo nyeti ya uchumi ikiwemo bandari ya Dar es Salaam ipo kwetu.
“Hivyo diwani wa Temeke lazima awe mtu anayetambua tunu hizi na awe mwenye mawazo na fikra pana si kuwa kama diwani tu, ndiyo maana nasema kuna diwani na diwani wa Temeke,” amesema.
“Lipo tatizo la baadhi ya viongozi kudharau waliyoyasisi watangulizi wao na kuanza mipango mipya, hii hudhoofisha utendaji wao na kujikuta wanamaliza miaka yao mitano wakipanga mikakati tu na kuangushwa katika chaguzi zijazo. Anzieni walipoishia watangulizi wenu kwani ipo mipango tuliyoachiwa na baraza lililopita ambayo tunaendelea nayo,” amesema.
Kuhusu amana ya uongozi amesema, “ni aibu sana kiongozi muhusika kwenye kashfa na kauli za ubabaishaji, kwani wananchi wanajua ishara zote, kiongozi lazima awe mwaminifu na mwadilifu kwa wananchi,” amesema, akiwataka viongozi kuwa madaraja kati ya wananchi na changamoto zao.
Pia, amewatwisha mzigo wa changamoto za huduma muhimu za kijamii zikiwemo afya na elimu.
“Afya za watoto wetu na elimu yao ni jukumu lenu, nalipongeza baraza lililopita kwa kuamua na kujenga hospitali mbili katika wilaya yetu, sasa katika mpango wa miaka 10 wa manispaa kumaliza kero ya upungufu wa madarasa na kujenga hospitali tano mpya ni jukumu lenu, haya ndiyo tunayotaka diwani wa Temeke alale na kuamka akiyafikiria.
Akizungumza katika kikao hicho, Meya wa Manispaa hiyo, Uzairu Athumani amewataka madiwani hao kuhakikisha wanazingatia maelekezo yaliyotolewa ili kuharakisha maendeleo.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Jomaary Satura, ametoa rai kwa viongozi kufuatilia na kuhakikisha maeneo ya wazi ndani ya wilaya hiyo yanasimamiwa na kutumiwa kikamilifu.
“Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 halmashauri yetu ilikusanya Sh47 bilioni, lakini mwaka 2024/2025 tumekusanya Sh63 bilioni na matarajio yetu mwaka huu ni kukusanya Sh70 bilioni, hizi zote zinaonesha juhudi bora katika usimamizi wa mapato ndani ya manispaa yetu ambayo yanakwenda kuboresha huduma za wananchi,” amesema.