Kibaha. Wazalishaji wadogo mkoani Pwani wameunga mkono mpango wa usajili wa bidhaa chini ya nembo ya ‘Made in Tanzania’ wakisema unaongeza fursa za masoko, huku wakiomba kupunguzwa kwa gharama za usajili ili kuwajumuisha wengi zaidi.
Wito huo umetolewa leo Februari 10, 2026, Kibaha, wakati wa mkutano wa wadau na wamiliki wa viwanda mkoani Pwani ulioandaliwa na Mamlaka ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa lengo la kuhamasisha usajili wa bidhaa na huduma na matumizi ya nembo ya ‘Made in Tanzania’.
Wamesema mpango huo ni mzuri na wenye tija kwa maendeleo ya viwanda vya ndani, lakini unahitaji maandalizi ya kifedha kwa wazalishaji wadogo.
Akizungumza kwenye mkutano huo mfanyabiashara Rahmat Abass amesema gharama ya Sh60,000 kwa kila bidhaa ni changamoto kwa wajasiriamali wanaozalisha bidhaa zaidi ya moja.
Washiriki wa Mkutano huo uliofanyika leo Kibaha Mkoa wa Pwani. Picha na Sanjito Msafiri
Amesema mjasiriamali anaweza kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo sabuni, karanga, juisi na batiki, hivyo kulazimika kusajili kila bidhaa kwa gharama tofauti kunapunguza hamasa ya kushiriki kikamilifu katika mpango huo.
Kwa upande wake, Jackson John ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama angalau kufikia kiwango cha Sh30,000 kwa kila bidhaa au kuweka utaratibu rafiki zaidi ili kuwahamasisha wazalishaji wadogo kushiriki.
Akizungumza kuhusu faida za kusajili biashara na kupata nembo ya ‘Made in Tanzania’, Meneja wa Kitengo cha Kujenga Uwezo na Ushauri wa TanTrade, Boniface Mrema amesema nembo hiyo inaongeza uaminifu wa bidhaa kwa walaji, inarahisisha upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi na kuitangaza Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Rehema Akida, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo, amesema Serikali ya Mkoa ipo tayari kutoa ushirikiano wa hali na mali ili kuhakikisha wazalishaji wanafanikiwa kusajili bidhaa zao na kupata nembo ya ‘Made in Tanzania’.
Washiriki wa Mkutano huo uliofanyika leo Kibaha Mkoa wa Pwani. Picha na Sanjito Msafiri
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na TanTrade kuwajengea uwezo wazalishaji, kukuza viwanda vidogo na kati na kuongeza mchango wa bidhaa za ndani katika uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.