AFCON 2027 YACHOCHEA MAENDELEO YA KILIMO KANDA YA KASKAZINI

Na Pamela Mollel,Arusha 

Maandalizi ya Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 yameibua fursa mpya za kukuza sekta ya kilimo katika Kanda ya Kaskazini, huku viongozi wakihimizwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula ili kukidhi mahitaji yatakayoongezeka wakati wa mashindano hayo.

Akifungua kikao kazi cha uhamasishaji na uendelezaji wa Shoroba za Kilimo leo Jumanne, Februari 10, 2026 Jijini Arusha, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, amesema ni wakati wa mikoa ya Arusha, Tanga, Kilimanjaro na Manyara kutumia rasilimali walizonazo kuzalisha chakula cha kutosha badala ya kutegemea mazao kutoka mikoa mingine.

Amesema AFCON 2027 italeta ongezeko kubwa la mahitaji ya chakula, hivyo ni muhimu viongozi na wataalamu wa kilimo kuandaa mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao, ajira kwa vijana na mapato ya wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo (ATO), Bi. Elizabeth Missokia, amesema maendeleo ya shoroba za kilimo yataunganisha uzalishaji, usindikaji, uhifadhi, usafirishaji na masoko, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kikao hicho kimefanyika katika Hoteli ya Mount Meru, Jijini Arusha, kikihusisha viongozi na wataalamu mbalimbali wa sekta ya kilimo kutoka ngazi za Mikoa na Halmashauri.