Geita. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Geita imefikisha mahakamani Mkurugenzi wa Matondo Breweries Investment Company Limited, Matondo Malanda wa Uyovu, Kata ya Buganzu, Wilaya ya Bukombe, akihojiwa kwa makosa manane ya kodi na forodha, ikiwemo uzalishaji wa pombe bila leseni inayostahili.
Malanda alipandishwa kizimbani Februari 10, 2026 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Cleophace Waane, na kusomewa mashtaka mbele ya Wakili wa Serikali, Emmanuel Fortunatus.
Katika shtaka la kwanza, anadaiwa kujihusisha na uzalishaji wa bidhaa zinazopaswa kulipiwa ushuru kinyume na Sheria ya Usimamizi wa Ushuru wa Bidhaa, Sura ya 147 toleo la 2023.
Mashtaka mengine ni kukutwa na bidhaa zisizolipiwa ushuru, kushindwa kuwasilisha taarifa sahihi, kubandika stempu za kughushi, na kuisababishia TRA hasara ya Sh81 milioni.
Anadaiwa kutenda makosa yote kati ya Machi 20, 2025 na Januari 2026. Malanda, akiwakilishwa na Wakili Beatus Emmanuel, alikana mashtaka yote.
Wakili wa Serikali aliomba tarehe nyingine ya shauri kwani upelelezi haujakamilika. Hakimu Waane amemrejesha Malanda rumande na kuahirisha kesi hadi Februari 25, 2026 itakapotajwa tena.
Meneja wa Idara ya Upelelezi wa Kodi Kanda ya Ziwa, Joel Mbilinyi, amesisitiza umuhimu wa wazalishaji kuwa na leseni halali, kutumia stempu za kielektroniki, na kuwahimiza wananchi kutoa taarifa pale wanapobaini bidhaa zinazodaiwa kughushiwa ili kulinda afya ya jamii na mapato ya Serikali.