Beki Dodoma Jiji arejea Uganda

ALIYEKUWA beki wa kushoto wa Dodoma Jiji, Dissan Galiwango, amesitisha mkataba wake wa miezi sita uliobakia na kikosi hicho, uliokuwa unaisha Juni 30, 2026, ambapo kwa sasa amejiunga na URA FC ya kwao Uganda kwa mkataba wa miaka miwili.

Galiwango aliyejiunga na Dodoma Jiji, Agosti 16, 2024, akitokea Kagera Sugar, alisaini mkataba wa miaka miwili na kikosi hicho cha ‘Walima Zabibu’, ingawa baada ya kubakia miezi sita aliomba kuondoka ili akapate changamoto sehemu nyingine.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Dodoma Jiji, umeliambia Mwanaspoti Galiwango alikuwa bado ana mkataba na kikosi hicho hadi mwisho wa msimu huu wa 2025-2026, ingawa baada ya kuomba kuondoka mwenyewe waliridhia ili akapate changamoto mpya.

Awali, mabosi wa Express ya Uganda pia aliyowahi kuichezea walifungua mazungumzo ya kumuhitaji beki huyo, ingawa URA FC imeinasa saini yake na kumrejesha, baada ya kucheza Ligi Kuu Bara katika kiwango kizuri tangu alipotua mara ya kwanza.

Nyota huyo aliwahi kuichezea Express mwaka 2018, baada ya kuachana na Saints Mukono, huku akichezea pia timu mbalimbali za UPDF FC na Vipers zote za kwao Uganda, ambapo kwa sasa mabosi wa kikosi hicho cha URA FC wamemrudisha tena nyumbani.

Licha ya kucheza tu beki wa kushoto, Galiwango alikuwa na mchango mkubwa tangu atue katika Ligi Kuu Bara, akianzia kwa Kagera Sugar na hadi Dodoma Jiji, huku akionyesha kiwango kizuri kwenye uzuiaji na wakati huohuo pia timu ikishambulia.