LICHA ya kumaliza duru la kwanza kileleni Ligi Kuu Bara, kipa wa JKT Tanzania, Ramadhan Chalamanda amesema hawajafikia malengo na mkakati wao ni kumaliza msimu huu nafasi tatu za juu, huku akichekelea rekodi.
Maafande hao wamekuwa bora msimu huu ambapo majuzi waliizima Mashujaa 1-0 na kukamilisha mechi 15 duru la kwanza kileleni wakiwa na pointi 27.
Msimu uliopita, timu hiyo hadi kumaliza raundi ya kwanza ilikuwa na pointi 24 kisha kumaliza msimu nafasi ya sita na alama 36
Majuzi dhidi ya Mashujaa ilishinda bao 1-0, huku Chalamanda akifikisha mechi tisa mfululizo golini ikipoteza mchezo mmoja dhidi ya Dodoma Jiji 1-0 ambayo ni rekodi mpya kwa kipa huyo.
Akizungumza na Mwanaspoti alisema hawajafikia malengo waliyojiwekea kila mechi kuvuna pointi tatu na sasa wanajiandaa na dhidi ya Coastal Union Februari 13, ambapo hesabu ni kusaka ushindi ili kujiimarisha zaidi kileleni.
“Tunashukuru kwa matokeo haya japokuwa mipango ilikuwa kuvuna pointi 40 kwa mechi 15 za mzunguko wa kwanza. Kwa kuwa ligi ina ushindani bado hatujapoteza mwelekeo na lolote linawezekana,” alisema Chalamanda.
Kuruhusu mabao tisa katika mechi 15, Chalamanda alisema sio hesabu nzuri na katika mechi zijazo anataka kumaliza ligi kwa wastani mzuri ili kusaka heshima ya mchezaji bora wa Ligi Kuu.