Dk Nguvila awataka watendaji Arusha kukuza utalii, aonya urasimu

Arusha. Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dk Toba Nguvila, amewataka watendaji wa Serikali mkoani humo kuzingatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza sekta ya utalii, akieleza kuwa ndiyo mhimili mkuu wa uchumi wa mkoa huo.

Akizungumza leo Jumatano, Februari 11, 2026, katika Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa, jijini Arusha, mbele ya watumishi wa ofisi hiyo na watendaji kutoka halmashauri za wilaya waliomlaki baada ya kuapishwa, Dk Nguvila amesema Arusha inabeba takribani asilimia 80 ya utalii na mikutano ya kimataifa nchini.

“Mheshimiwa Rais alisisitiza umuhimu wa utalii. Arusha ndiyo kitovu cha sekta hii, hivyo ni wajibu wa watendaji kuwezesha uwekezaji badala ya kuweka vikwazo,” amesema.

Ameonya dhidi ya urasimu unaoweza kukwamisha wawekezaji, akisisitiza kuwa heshima ya Arusha inatokana na utalii na karibu kila wilaya ina vivutio vya utalii. Pia amezitaka halmashauri kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo.

“Hatuwezi kuona halmashauri zinatenga fedha kidogo kwa utalii wakati ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wetu,” amesema.

Dk Nguvila pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kazini, akionya kuwa hatavumilia migogoro miongoni mwa viongozi na watendaji wa taasisi za umma.

“Hatutaki migogoro kati ya viongozi wa taasisi au kati ya Katibu Tawala Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri. Migogoro haina faida, tufanye kazi kwa ushirikiano,” amesema.

Ameelekeza viongozi kuwa na mpango wa kushughulikia kero za wananchi kwa wakati na kupimwa kwa uwezo wao wa kuzitatua. Amewataka kutoka maofisini na kwenda kwa wananchi kusikiliza na kutatua changamoto zao.

Aidha, amesisitiza watumishi kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni (STK) katika utendaji wao, akionya kuwa ukiukwaji unaweza kuwagharimu hata baada ya kustaafu.

Kuhusu Bima ya Afya kwa Wote, amesema ni ahadi muhimu ya Rais Samia na kwamba Arusha inaongoza kitaifa kwa uandikishaji, lakini juhudi zinapaswa kuendelea ili kulinda nguvu kazi ya wananchi.

Dk Nguvila pia amewataka watendaji wa wilaya za mipakani kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na nchi jirani huku wakidhibiti migogoro ya wafugaji wanaoingiza mifugo bila kufuata sheria.