Dk Warsame, wenzake kizimbani kwa mashitaka 841

Mwanza. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza imemshtaki Mkurugenzi na mmiliki wa kampuni ya Salaaman Health Services Ltd, Dk Abdi Warsame na mwenzake, Ofisa Rasilimali Watu, Elia Makongwa kwa makosa 841 ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Februari 10, 2026 wakikabiliwa na mashtaka yanayojumuisha kuongoza genge la uhalifu, kughushi na kutumia nyaraka za uongo, wakidaiwa kupokea Sh1.011 bilioni huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la uhalifu.

Kwa mujibu wa upande wa Jamhuri, washtakiwa wanadaiwa kuusababishia Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) hasara ya zaidi ya Sh1 bilioni kati ya mwaka 2021 na 2023 kupitia genge la uhalifu lililokuwa likifanya kazi katika mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam.




Inadaiwa kuwa walighushi nyaraka za wagonjwa na kuzitumia kujipatia fedha isivyo halali kutoka ofisi za NSSF jijini Dar es Salaam kwa madai ya kutoa huduma za matibabu katika Kituo cha Afya cha Salaaman kilichopo mkoani Mwanza.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Erick Maley ameahirisha kesi hiyo namba 2330 ya mwaka 2026 hadi Februari 24, 2026 baada ya kutoa uamuzi mdogo kuhusu ombi la matibabu kwa mshtakiwa wa kwanza, Dk Abdi.

Ameelekeza mamlaka za magereza kuhakikisha mshtakiwa huyo anapatiwa huduma ya afya kwa mujibu wa taratibu.

Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea tena Februari 24, 2026 mahakamani hapo ambapo washtakiwa wamerudishwa rumande huku upande wa mashtaka, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Fadhiri Mwandolomo, ukiendelea na taratibu za kisheria kwa ajili ya uendeshaji wa kesi hiyo.