MABOSI wa Mashujaa wameanza mchakato wa kutafuta kocha mpya atakayekinoa kikosi hicho cha maafande, huku makocha wawili ambao ni Fikiri Elias na Fredy Felix ‘Minziro’, anayeifundisha kwa sasa Bigman FC ya Championship wakichuana pia vikali.
Hatua ya Mashujaa ya kusaka kocha huyo mpya, inajiri baada ya kuachana na Salum Mayanga, aliyeondoka baada ya kukiongoza kikosi hicho katika mechi 12, za Ligi Kuu Bara msimu huu, ambapo kati ya hizo alishinda tatu, sare nne na kuchapwa tano.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Mashujaa, zimeliambia Mwanaspoti makocha, Fikiri Elias na Fredy Felix ‘Minziro’, ndio wanaopewa zaidi nafasi ya kurithi mikoba ya Mayanga, japo hadi sasa hakuna muafaka uliofikiwa juu ya hilo.
“Kwa sasa suala hilo liko katika uongozi wa juu wa kufanya uamuzi wa mwisho, ingawa ni kweli makocha, Fikiri na Minziro, ndio wanaochuana katika nafasi hiyo ya kuiongoza timu yetu, hilo ndilo ninaloweza kulielezea,” kilisema chanzo hicho.
Kocha, Fikiri hana timu yoyote kwa sasa tangu alipoachana na KenGold, Septemba 17, 2024, kwa makubaliano ya pande mbili, huku kwa Minziro anayeifundisha Bigman FC, akipita pia, Geita Gold, Pamba Jiji na Tanzania Prisons.
Mbali na Mashujaa iliyomuhitaji, Minziro, kocha huyo mzoefu pia anapigiwa hesabu na timu ya Soka ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA SC) inayoshiriki Ligi Daraja la Pili (First League), akachukue nafasi ya John William Zongwe, aliyeondoka.
Mayanga alijiunga na Mashujaa FC Machi 21, 2025, akitokea Mbeya City, akienda kuchukua nafasi ya Kocha, Abdallah Mohamed ‘Baresi’, ikiwa ni muda mfupi baada ya kikosi hicho kuchapwa mabao 3-0, dhidi ya Singida Black Stars, Februari 26, 2025.
Baada ya kuondoka Mayanga aliyeifundisha pia Mtibwa Sugar, timu hiyo inaongozwa na Kocha msaidizi, Charles Fred ambaye katika mechi mbili za Ligi Kuu, alianza na suluhu (0-0) dhidi ya Tanzania Prisons kisha kuchapwa na JKT Tanzania bao 1-0.