Kauli ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi, kuhusu matukio ya Oktoba 29, 2025, imethibitisha kwa vitendo kuwa Serikali ni sikivu na iko tayari kupokea ushauri mzito unaolenga maslahi mapana ya taifa, hata pale unapokuja kwa namna ya “kidonge kichungu”.
Katika maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, Makamu wa Rais alikubaliana waziwazi na hoja zilizotolewa na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, akitoa wito wa kuacha kuendelea kuyazungumzia hadharani matukio ya Oktoba 29, 2026 ili kutoa nafasi kwa Tume ya Uchunguzi kufanya kazi yake kwa uhuru na kwa misingi ya kisheria.
Kauli hiyo imepokelewa kama ishara muhimu ya unyenyekevu wa uongozi na utayari wa Serikali kusikiliza sauti za wadau, hususan taasisi za kitaaluma na kisheria, katika nyakati nyeti kwa mustakabali wa taifa.
Kwa muktadha huo, pongezi za dhati zinastahili kutolewa kwa Makamu wa Rais kwa kuonyesha mfano wa uongozi unaotanguliza hekima, busara na maslahi ya taifa.
Vilevile, pongezi zinamstahili Wakili Boniface Mwabukusi kwa ujasiri wake wa kuzungumza mambo mazito, muhimu na ya msingi kwa mustakabali wa nchi, kwa lugha ya uwazi na uwajibikaji.
Kauli yake imeonesha nafasi ya TLS kama taasisi yenye wajibu wa kusimamia misingi ya katiba, sheria na haki bila woga wala upendeleo.
Kwa upande wa waandishi wa habari na wachambuzi wa masuala ya umma, ni jambo la kujivunia pale hoja wanazoandika au kuzitoa zinapothibitishwa na viongozi wakuu wa nchi.
Ni faraja na uthibitisho kuwa uandishi wenye dhamira njema unaweza kuchangia mabadiliko chanya katika uongozi na utawala wa nchi.
Ikumbukwe kuwa, katika makala ya salamu za Mwaka Mpya iliyowahi kuchapishwa awali, nilishauri Serikali iwajibike kwa yaliyojiri Oktoba 29 na Watanzania kuacha kubaki kwenye machungu ya tukio hilo, badala yake kushirikiana na Tume ya Uchunguzi ili ipate fursa ya kuja na majibu yatakayosaidia uponyaji na maridhiano ya kitaifa. Kauli ya Makamu wa Rais sasa imeipa uzito hoja hiyo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Makamu wa Rais alisisitiza kuwa wito wa kunyamaza kuhusu tukio hilo hauwahusu viongozi wa Serikali pekee, bali pia viongozi wa vyama vya siasa, taasisi za kiraia na wanaharakati.
Lengo ni kuepuka kutonesha vidonda vya taifa na kulinda mchakato wa haki unaoendelea chini ya vyombo halali vya kisheria.
TLS, kupitia Rais wake, ilitoa rai kwa viongozi kuwa waangalifu na kauli wanazozitoa kwa wananchi, ikisisitiza misingi ya kusema ukweli, haki, uwazi na uwajibikaji kama njia ya kurejesha matumaini na mshikamano wa kitaifa.
Wakili Mwabukusi alinukuu maneno ya Alex Boraine akisisitiza kuwa msamaha wa kweli hauwezi kupatikana bila uwajibikaji, na kwamba, kufumbia macho makosa si suluhu bali ni kupuuza haki.
Katika busara zake, alikumbusha hekima ya Kiswahili isemayo ‘ukivuliwa nguo, chutama’, akieleza umuhimu wa unyenyekevu na tahadhari katika nyakati za majaribu ya kitaifa, ili taifa lisipoteze mwelekeo.
Kwa mtazamo huo, kauli ya Makamu wa Rais aliyetoa akiwa anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika maadhimisho yaliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli jijini Dodoma, imeonesha dhamira ya dhati ya Serikali kukubali ushauri wa kisheria na kuuenzi utawala wa sheria.
Hata hivyo, kama mwanachama hai wa TLS, bado ipo haja ya chama hicho na taasisi nyingine za kisheria kuwa mstari wa mbele zaidi katika kukemea uvunjifu wowote wa Katiba, sheria na taratibu pindi unapotokea, bila kusubiri majukwaa maalum.
Aidha, mhimili wa Mahakama, kama mlinzi mkuu wa Katiba, una wajibu wa kutumia mamlaka yake pale inapobidi, hata kwa misingi ya suo moto, kulinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa jumla, hatua ya Serikali kuonyesha sikivu kwa kuzingatia ushauri wa TLS ni somo muhimu la uongozi na demokrasia.
Ni mwanzo mzuri wa kujenga taifa linalosikilizana, kuwajibika na kusonga mbele kwa umoja.