INSPECTOR ABEL AWASHUKURU WADAU WA HABARI, TAFITI YAKE KULETA MATOKEO CHANYA

::::::::

Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Abel Paul, ametoa shukrani za dhati kwa wadau wote wa sekta ya habari kwa ushirikiano wao mkubwa uliowezesha kukamilika kwa utafiti wake wa kitaaluma. Kwa namna ya kipekee, ameishukuru Clouds Media Group (CMG), Millard Ayo pamoja na wanahabari na watumishi wote wa vyombo vya habari kwa mchango wao muhimu katika kufanikisha zoezi hilo.

Abel amesema kuwa ushirikiano huo ulikuwa nguzo imara katika kukamilisha utafiti huo, hasa ukizingatia unyeti na nafasi kubwa ya sekta ya habari katika jamii. Ameeleza kuwa utafiti huo ulikuwa sehemu ya mahitaji ya shahada ya uzamili katika masuala ya ulinzi wa taarifa na utawala bora, ambapo alijikita kuchambua kwa kina usalama wa taarifa, maadili ya taaluma ya habari, pamoja na mifumo ya uwazi na uwajibikaji.

Aidha, ameeleza kuwa matokeo ya utafiti wake yamekuja na mapendekezo ya kitaalamu yatakayosaidia kuboresha uendeshaji na uripoti wa masuala ya kihabari, si tu nchini Tanzania bali pia kimataifa. Amebainisha kuwa utafiti huo umejibu baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya habari na kutoa dira ya maboresho yenye tija kwa wadau wote.

Akihitimisha, Abel amesisitiza kuwa maarifa na matokeo ya utafiti huo yatatumika kama nyenzo muhimu katika kuimarisha ulinzi wa taarifa, kukuza mawasiliano yenye tija, na kuendeleza misingi ya utawala bora kwa maendeleo endelevu ya jamii.

@abelstanfordp ✍️✍️