Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amewataka wananchi kusajiliwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) ili kunufaika na huduma zinazotolewa kupitia mifumo inayohusiana na mamlaka hiyo.
Akizungumza alipofanya ziara makao makuu ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), jijini Dar es Salaam, Katambi amesema kusairiwa kwenye mfumo huo kutasaidia kuondoa usumbufu katika huduma mbalimbali.
“Kitambulisho cha Taifa kinafungua mlango wa huduma nyingi muhimu, zikiwemo matibabu, kujiunga na vyuo vya elimu ya juu, kupata huduma za umeme na maji, huduma za kibenki, hati za kusafiria, leseni za magari na biashara.
“Utoaji wa Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN), usajili wa kampuni binafsi, na huduma kwenye mifuko ya kijamii kama vile mafao ya kustaafu na fidia za ajira,” amesema.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Nida, James Kaji amesema mamlaka hiyo inaendelea na jitihada za kutatua changamoto za majina kwa wananchi wenye sababu halali baada ya kuwasilisha nyaraka muhimu.
Amebainisha kuwa jitihada hizo zinajumuisha wale waliopata msamaha wa Rais Samia Suluhu Hassan, unaowawezesha kurekebisha rekodi zao, ili taarifa zao za Nida zionyeshe majina yao halisi badala ya yale yaliyoonekana kwenye vyeti bandia vya kitaaluma kwenye ngazi mbalimbali.
Aidha, amewataka wananchi ambao bado hawajachukua vitambulisho vyao kutika ofisi za Nida wilayani wafanye hivyo ili waanze kuzitumia kupata huduma mbalimbali.