Kibu afuata mamilioni yake Libya

WIKI moja iliyopita, gazeti hili lilifichua kufikiwa kwa makubaliano baina ya Simba na Al Nasr ya Libya juu ya uhamisho wa mshambuliaji Kibu Denis kwa dau la Dola 300,000 (Sh776 milioni).

Baada ya makubaliano hayo kilichobakia kilikuwa ni mazungumzo binafsi baina ya Kibu na Walibya hayo kwa ajili ya maslahi yake binafsi ambayo yalikuwa yanangojea mshambuliaji huyo ambaye pia anaichezea timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ arejee kutoka Angola ambako Simba ilikuwa na mchezo wa ugenini wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro Luanda uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Sasa baada ya Simba kurejea, upande wa Kibu juzi usiku ulikutana na ule wa Al Nasr na kufikia makubaliano ambayo yamekamilisha mchakato wa usajili wa nyota huyo ambaye muda wowote kuanzia sasa atatangazwa kuwa mchezaji wa Al Nasr.

Katika makubaliano hayo, timu hiyo ya Libya imemuwekea kitita kikubwa cha fedha ambacho kiuhalisia ingekuwa ngumu kwa nyota huyo wa zamani wa timu za Mbeya City, Geita Gold na Kumuyange kukataa kujiunga nayo.

Mbali na Sh776 milioni ambazo Simba itaingiza kwa kumuuza Kibu Denis ambaye mkataba wake ulibakiza miezi sita, mshambuliaji huyo yeye binafsi atapata kiasi cha Dola 700,000  (Sh1.8 bilioni) katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu ambacho atautumikia mkataba wa timu yake mpya.

Katika fungu hilo la fedha ambalo Kibu Denis atapata, kiasi cha Sh900 milioni atakuwa akilipwa kama stahiki za mshahara na bonasi ambapo kila mwezi atakuwa akipokea kitita cha Sh50 milioni.

Kiasi kilichobakia ambacho ni Sh900 milioni, ni ada ya kusaini ambayo mchezaji huyo atapewa na kwa mujibu wa chanzo cha uhakika kilicho karibu na mchezaji huyo, fungu hilo lote atapewa taslimu mara baada ya kutambulishwa rasmi.

Chanzo hicho kimethibitisha kwamba mchezo baina ya KMC na Simba leo kwenye Uwanja wa  KMC Complex utakuwa wa mwisho kwa mchezaji huyo na atautumia kuaga mashabiki wa Simba.

Msimamizi wa Kibu Denis, Carlos Sylivester amesema kuwa taarifa zozote kuhusu mshambuliaji huyo zitatolewa na Simba.

“Waajiri wa Kibu Denis ni Simba hivyo wao kama kuna lolote linalomhusu mchezaji ndio wanaweza kutoa ufafanuzi,” amesema Sylivester.

Kibu Denis ameitumikia Simba kwa miaka minne na nusu tangu alipojiunga nayo mwaka 2021 akitokea Mbeya City.

Al Nasr inaongoza msimamo wa kundi namba nne la Ligi Kuu ya Libya ikiwa na pointi 21 ilizokusanya baada ya kuibuka na ushindi katika mechi zote saba ilizocheza.

Msimu huu Kibu Denis ameifungia Simba mabao mawili yote yakiwa ni katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mabao hayo aliyafunga katika mechi ya raundi ya kwanza dhidi ya Nsingizini Hotspurs ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0. Ndani ya Al Nasr, Kibu atakutana na nyota wawili aliocheza nao Simba hivi karibuni ambao ni kiungo Fabrice Ngoma na mshambuliaji Steven Mukwala.

Katika hatua nyingine, ukiondoa mchezo baina ya Simba na KMC leo kuanzia saa 1:00 usiku, kutakuwa na mchezo mwingine wa ligi hiyo baina ya Singida Black Stars na Fountain Gate itakayochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex kuanzia 10:00 jioni.