Dar/Dodoma. Uendeshaji wa pikipiki na bajaji za umeme pasipo kusajiliwa katika miji ya Dar es Salaam na Dodoma umechangiwa na utekelezaji duni wa sheria za usafiri na usajili, uchunguzi wa Mwananchi umebaini.
Ingawa Tanzania imefanya marekebisho ya sheria ili kutambua rasmi magari ya umeme (EVs), upungufu mkubwa wa utekelezaji umeruhusu maelfu ya pikipiki na bajaji za umeme kufanya kazi kwa uhuru kwenye barabara za umma bila usajili, namba za usajili au bima.
Ukuaji huo usiodhibitiwa wa vyombo hivyo, unazua hofu ya usalama wa umma na Taifa kwa jumla, huku ukiinyima Serikali mapato kiasi kikubwa cha mapato.
Mwananchi ilifanya uchunguzi katika miji ya Dar es Salaam na Dodoma kati ya Oktoba na Desemba 2025 ili kubaini ukubwa wa tatizo hilo na kupendekeza namna bora ya kurekebisha hali hiyo ili kuimarisha usalama wa umma na kuongeza mapato ya Serikali kwa maendeleo ya Taifa.
Uchunguzi ulibaini kuwepo kwa tatizo la usimamizi na udhibiti wa vyombo hivyo, mifumo finyu ya ufuatiliaji na matumizi duni ya sheria miongoni mwa taasisi zinazohusika katika kukabiliana na tatizo hilo.
Matokeo yake, pikipiki na bajaji za umeme zimeendelea kufanya kazi waziwazi katika majiji hayo bila uwajibikaji, jambo lililosababisha idadi yake kuongezeka kwa kasi.
Uchunguzi umeonesha kuwa, awali baadhi ya waagizaji walitangaza kuingiza pikipiki na bajaji za umeme kama vipuri, lakini baadaye waliziunganisha nchini kisha kuziingiza kwenye matumizi ya usafiri na usafirishaji.
Utaratibu huu unavuruga mchakato wa usajili, pia unadhoofisha utiifu wa kisheria na kuleta ugumu wa kubaini kama vyombo hivyo, vinapaswa kufanya kazi kwenye barabara za umma.
Mamlaka zinazohusika na utekelezaji zimeshindwa kuchukua hatua dhidi ya vyombo hivyo au kuwawajibisha wamiliki na waendeshaji kwa kutofuata sheria, jambo linalokuza tatizo hilo.
Hata hivyo, taasisi muhimu ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Polisi wa Usalama Barabarani na Jeshi la Polisi, zimekuwa zikirushiana mpira kuhusu kuongezeka kwa pikipiki na bajaji za umeme zisizosajiliwa nchini.
Hali hiyo katika taasisi hizo muhimu, inaongeza hatari za usalama na kupunguza mapato kutokana na ada za usajili na leseni ambazo hazikusanywi, pamoja na faini na adhabu ambazo hazijakusanywa.
Hii ni kinyume na Kifungu cha 57(b)(I–IV) cha Sheria ya Marekebisho ya Kodi ya Usajili na Uhamisho wa Magari, Sura ya 124 ya mwaka 2023, kinachotambua uwepo wa vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati ya umeme ikiwa ni pamoja na pikipiki na bajaji katika mfumo wa kisheria wa Tanzania.
Pia, inakiuka Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, hasa Kanuni za Marekebisho ya Usajili wa Magari ya 2025, zilizoanzisha vifungu vidogo 1A(a)–(d).
Vifungu hivi vinaweka ada za leseni za magari zinazotozwa wakati wa utoaji wa cheti cha usajili kwa vyombo vinavyotumia umeme.
Ada hizo zimegawanywa katika makundi matatu: EVs za Nguvu Ndogo (chini ya 50kWh), EVs za Nguvu ya Kati (50.1–100kWh) na EVs za Nguvu Kubwa (100.1–200kWh).
Kanuni hizo, zilizotangazwa rasmi Juni 26, 2025 na kutiwa saini na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, zinaweka ada za usajili za Sh50,000, Sh200,000 na Sh250,000 kwa madaraja ya 1, 2 na 3 mtawalia, huku Sh300,000 zikihusika kwa EVs za utendaji wa juu.
Kifungu kidogo cha 1B kinaeleza kuwa, ada ya leseni ya pikipiki, iwe ya umeme au ya kawaida, ni Sh30,000, wakati ile ya bajaji inayobeba mizigo au abiria ni Sh50,000.
Hata hivyo, Kifungu cha 13(1) na (2) cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, kinakataza matumizi ya gari au trela yoyote kwenye barabara za Tanzania pasipo kusajiliwa.
Kifungu cha 13(2) kinasema kwamba, mmiliki au dereva yeyote anayeendesha gari lisilosajiliwa anafanya kosa, hivyo kustahili faini isiyozidi Sh50,000, kifungo cha hadi miaka mitano, au vyote viwili, na chombo chake kinaweza kutaifishwa na Serikali.
Hali ya sasa pia inakiuka Mpango Mkakati wa Taifa wa Usalama Barabarani wa 2024/25 na 2026/27 na ahadi ya Tanzania katika Muongo wa Dunia wa Hatua za Usalama Barabarani 2021–2030.
Pia, Umoja wa Mataifa kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO) umelenga kupunguza vifo na majeruhi wanaotokana na ajali za barabarani kwa angalau asilimia 50 ifikapo 2030.
Uchunguzi umebaini kuwa pikipiki na bajaji nyingi za umeme zinatumika kusafirisha abiria na mizigo, hasa katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu ambao ni ngumu kufikiwa na usafiri wa kawaida au ghali.
Hata hivyo, vyombo vingi vimebainika kukosa namba za usajili au sahani za namba hizo, hali inayoongeza ugumu kwa mamlaka kufuatilia na kuwawajibisha wamiliki au waendeshaji endapo ajali au uhalifu utatokea.
Watumiaji waliohojiwa walikiri kufahamu mahitaji ya usajili wa vyombo vyao na kubainisha kuwa, utekelezaji dhaifu wa sheria umewahamasisha kutotii sheria.
Baadhi ya waendeshaji wamesema kusajili vyombo vyao hakuwalipi kwani wameona wenzao kadhaa wakinufaika kwa kuendesha vyombo vyao pasipo usajili wala bima.
Wataalamu wa sheria wanaonya kuwa kukosekana kwa namba za utambulisho inaleta ugumu kufuatilia vyombo vinavyohusika katika matukio ya ajali na uhalifu.
Wamesema, kukosekana kwa bima kunawaacha abiria, madereva na watumiaji wengine wa barabara katika hatari endapo watajeruhiwa au kupoteza maisha.
Wamebainisha kuwa, katika nchi za India na China wameanzisha mifumo ya wazi ya usajili vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati ya umeme, ikiwamo namba maalumu zinazorahisisha utambuzi kwa maofisa wanaohusika na utekelezaji.
Mifumo hii, wamesema imeimarisha utii wa sheria huku ikihamasisha matumizi ya usafiri ambao ni rafiki kwa mazingira.
Wachambuzi wa masuala ya usafiri wanasema Tanzania ingeweza kujifunza kutoka mataifa hayo wakati wa kurekebisha sheria zake za kutambua magari ya umeme.
Wanasema sheria hazipaswi tu kutambua teknolojia mpya bali ziambatane na mifumo thabiti ya utekelezaji inayozingatia mabadiliko ya sekta ya usafiri.
Hata hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Sheria cha Polisi Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Mussa Manyama anasema polisi wanawajibika kukamata magari yasiyosajiliwa kupitia operesheni endelevu za utekelezaji.
Anakiri kuwa, kuendesha gari lisilosajiliwa, iwe la umeme au la kawaida, ni ukiukaji wa sheria na kunaleta hatari kubwa kwa usalama wa umma.
Manyama anasema magari hayo kwa kawaida hayana bima, hivyo kuwaweka madereva, abiria na watumiaji wengine wa barabara katika hatari kubwa endapo ajali itatokea, na kwamba wakiukaji wanapaswa kutozwa faini kali, kufikishwa mahakamani na kutaifishiwa magari yao.
Hata hivyo, alikataa kutoa takwimu kuhusu idadi ya magari ya umeme yasiyosajiliwa ambayo yametozwa faini, kutaifishwa au kuondolewa barabarani tangu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilipotangaza tarehe ya mwisho ya usajili, Juni 2025.
“Tutaendelea kutekeleza sheria na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa usajili,” anaema bila kutoa matokeo mahususi ya utekelezaji.
Wataalamu wa sheria wamekosoa kile walichokiita kurushiana mpira kitaasisi, wakihimiza mamlaka kuacha kukwepa wajibu na badala yake kusimamia utekelezaji wa sheria kama inavyoelekezwa.
Mwanasheria kutoka Divina Attorneys, Edson Kilatu, anasema hali hiyo inaonesha kuongezeka kwa utamaduni wa kutojali sheria na uwajibikaji duni miongoni mwa mamlaka na wananchi.
“Hii ni hatari sana. Ajali zinapotokea na kesi kufika mahakamani, mara nyingi ushahidi wa kutosha unakosekana. Katika baadhi ya matukio, hata inakuwa ngumu kupata utambulisho wa gari husika,” anasema.
Kilatu alisisitiza kuwa, ni jukumu la mamlaka kuhakikisha utekelezaji madhubuti wa sheria, ikiwamo kutoa matangazo ya wazi na kwa wakati kwa umma, ili kuboresha utii wa sharia nchini.
Mwanasheria mwingine ambaye anaomba kutotajwa gazetini alisema tatizo halipo kwenye sheria bali utekelezaji wake.
Chanzo hicho kinaeleza kuwa, utekelezaji madhubuti unahitaji ushirikiano wa wananchi wote, si polisi pekee, ingawa polisi ndio wenye mamlaka ya kuhoji na kukamata wahalifu.
Chanzo kinabainisha kuwa, polisi mara nyingi hutegemea taarifa kutoka kwa umma ili kuchukua hatua dhidi ya ukiukaji fulani, na kwamba katika baadhi ya matukio huenda wasichukulie makosa kama kuendesha gari bila namba kama ni tatizo kubwa.
“Kuna haja ya elimu endelevu kwa umma kuhusu matumizi ya magari ya umeme ili wananchi waelewe umuhimu wa kufuata sheria,” kinasema chanzo hicho.
Kuhusu Jeshi la Polisi, chanzo hicho kiliendelea kusema, linaweza pia kuhitaji mafunzo maalumu kuhusu magari ya umeme ili kuongeza uelewa kuhusu uhibiti, hatari na mahitaji ya utekelezaji.
Hivyo askari wa usalama barabarani, polisi, TRA na mamlaka zingine za Serikali lazima washirikiane kikamilifu ili kulinda usalama, mapato na usalama wa watumiaji wote wa barabara kwa manufaa ya mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa jumla.