WAKATI Coastal Union ikichekelea kurejea kwa nyota wake waliokuwa majeruhi, straika wa timu hiyo Maabad Maulid amesema kwa sasa anajitathimini alipokwama ili kurejesha kasi yake ya kufunga mabao Ligi Kuu.
Coastal haikuwa na mwanzo mzuri Ligi Kuu baada ya kucheza mechi saba mfululizo bila kuonja ushindi kabla ya juzi kuamka na kuikanda Tanzania Prisons kwa mabao 4-1 na kuchumpa nafasi ya tisa kwa pointi 14 baada ya michezo 14.
Hata hivyo, licha ya matokeo hayo, Maabad aliyetua kikosini humo akitokea KVZ ya Zanzibar akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu visiwani humo msimu wa 2020/21 kwa mabao 17 kwa sasa amefunga mabao mawili tu.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mohamed Muya amesema licha ya kusota kwa muda mrefu bila matokeo mazuri, tatizo lilikuwa kwa baadhi ya mastaa wake ambao walikuwa na majeraha na kuipa wakati mgumu benchi la ufundi kutengeneza muunganiko.
Amesema wachezaji kama Masumbuko Othman ‘Makambo Jr’, Meshack Mwamita, Maabad Maulid, Cleopahas Mkandala na safu nzima ya ushambuliaji hawakuwapo kutokana na majeraha ila kwa sasa wamerejea wote.
“Kwa maana hiyo ile presha yetu itapungua kiasi fulani, tunaamini kuanzia ushindi huu dhidi ya Prisons tutaanza upya, kiujumla niwashukuru mashabiki na uongozi kwa kutuvumilia, lakini wachezaji wanavyopambana,” amesema kocha huyo.
Kwa upande wa Maabad, amesema mabao mawili aliyonayo si mwendelezo mzuri kama mshambuliaji akieleza kuwa anaenda kujitathimini alipokosea na kurejesha kasi yake upya.
Amesema kwa sasa anapitia kipindi kigumu na kwamba matokeo ya jumla kwa timu yaliwapa ugumu wachezaji akiahidi kuwa anaendelea kusaka mabao Ligi Kuu na kuwaomba mashabiki kutowakatia tamaa.
“Napitia wakati mgumu japokuwa nyakati hazifanani, kuna muda unapanda au kushuka, mabao mawili kama straika siyo kitu kizuri tunapambania timu ipate matokeo mazuri na ninaendelea kutafuta mabao,” amesema Straika huyo.
Katika mechi ya jana, Coastal ilipata mabao yake kupitia kwa Bakar Msimu aliyefunga mawili likiwamo la sekunde ya 58 tangu kuanza kwa pambano likiwa bao la mapema zaidi, kisha Shiza Kichuya aliyetua hivi karibuni akifunga la tatu kabla ya Mkandala kuongeza chuma cha nne.