Mabadiliko ya tabianchi yaibua hofu kwa watu wenye ulemavu

Dar es Salaam. Wakati athari za mabadiliko ya tabianchi zikizidi kushuhudiwa kwa mafuriko, ukame na uhaba wa maji katika Jiji la Dar es Salaam, kundi la watu wenye ulemavu limeendelea kuwa miongoni mwa waathirika wakubwa zaidi lakini mara nyingi sauti zao hazisikiki katika mipango ya kukabiliana na changamoto hizo.

Hali hiyo imeibuka wakati wa mjadala uliofanyika katika Kata ya Kawe, Wilaya ya Kinondoni, ambako jamii imekutana kujadili kwa kina namna mabadiliko ya tabianchi yanavyowaathiri makundi hatarishi na nini kifanyike.

Mdahalo huo uliofahamika kama Mgahawa wa Maarifa, uliwakutanisha wanawake, wazazi, vijana, viongozi wa jamii pamoja na watu wanaoishi na ulemavu kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kutafuta suluhisho la pamoja.

Tukio hilo liliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la MyLEGACY kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania kupitia Mradi wa Kesho Njema, likilenga kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi, hasa kwa wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mwenyekiti wa Kikundi cha Wajasiriamali Walemavu Kawe (Wawaka) Mrisho Bilal amesema watu wenye ulemavu kwa muda mrefu wamekuwa wakiachwa nje ya mijadala ya tabianchi licha ya kuwa katika hatari kubwa wakati wa majanga.

“Kwa muda mrefu watu wenye ulemavu tumekuwa tukiachwa nje ya mijadala ya tabianchi, ilhali sisi ndiyo tunaathirika zaidi wakati wa mafuriko, ukame au majanga mengine. Leo tumepata nafasi ya kusema na kusikilizwa,” amesema Bilal.

Washiriki mbalimbali wakifuatilia mdahalo wa kukuza uelewa juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa watu wenye ulemavu.



Kupitia majadiliano ya wazi, washiriki wameleza namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri maisha yao ya kila siku, kuanzia changamoto za upatikanaji wa maji hadi kuongezeka kwa hatari za ukatili wa kijinsia.

Mratibu wa Programu kutoka MyLEGACY, Amina Mtengeti, amesema Mgahawa wa Maarifa umebuniwa kama jukwaa salama la sauti za jamii, akisisitiza kuwa ustahimilivu wa tabianchi hauwezi kujengwa bila ushirikishwaji wa makundi yote.

“Hatuwezi kujenga ustahimilivu wa tabianchi bila kusikiliza sauti za wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu. Suluhisho lazima yatokane na jamii yenyewe,” alisema.

Akichangia mada kwenye mdahalo huo Mwajuma Ramadhani amesema uhaba wa maji unaotokana na mabadiliko ya tabianchi huongeza mzigo kwa wanawake, huku pia ukiwaweka katika hatari ya ukatili.

“Tunapokosa maji, sisi wanawake tunapata shida kutafuta maji. Hapo ndipo hatari ya ukatili inaanza, lakini mara nyingi hakuna mtu anayeliona hilo kama tatizo la tabianchi,” amesema Mwajuma.

Aidha, imelezwa kuwa wanawake wanaoishi na ulemavu au wanaolea watoto wenye ulemavu hukumbana na changamoto maradufu wakati wa majanga.

“Wanawake ndio tunabeba mzigo wa kutunza familia wakati wa ukame au mafuriko. Ukiongeza ulemavu au kuwa na mtoto mwenye ulemavu, mzigo unaongezeka lakini msaada hauongezeki,” amesema Regina Bwire.

Hatari zinazowakumba watu wenye ualbino pia ziliangaziwa, huku ikielezwa kuwa mgao wa maji huwafanya kwenda kutafuta maji usiku na hivyo kukumbana na hatari za mashambulizi.

Washiriki walibainisha kuwa katika hali za dharura kama mafuriko, watu wenye ulemavu mara nyingi huachwa nyuma kutokana na kukosekana kwa mifumo jumuishi ya uokoaji.

Mradi wa Kesho Njema unalenga kuunganisha masuala ya tabianchi, usawa wa kijinsia na haki za afya ya uzazi ili kujenga jamii salama na yenye ustahimilivu huku ukiwekwa msisitizo kuwa mabadiliko ya tabianchi si suala la mazingira pekee bali ni suala la haki na maisha ya watu hasa wale walio katika mazingira magumu zaidi.