Dar es Salaam. Inaumiza kiasi gani unawaacha watoto wako pacha wakiwa wazima katika chumba ulichopanga, unakwenda kwa wakala kutoa pesa, lakini unarudi unakuta watoto wamenyongwa, hili ndilo lililomkuta Mwajuma Milonge.
Jaji Hussein Mtembwa wa Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, amemwachia huru Milonge aliyeshitakiwa kwa mauaji ya wanawe, Sulaiya Kunembe na Suleiya Kunembe, huku Jaji akiwalaumu Polisi kuwa kesi hiyo haikuchunguzwa vya kutosha.
Tukio hilo la mauaji linadaiwa kutokea Septemba 28, 2024 katika eneo la Kisanga Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na kutokana na hukumu ya Jaji Mtembwa aliyoitoa Februari 6, 2026, swali linabaki, ni nani aliyewanyonga pacha hao.
Awali, maelezo ya kosa kabla ya Jaji kumwachia huru Milonge, yalidai siku hiyo, mama huyo maarufu kwa jina la ‘Mama Wawili’ kwa makusudi alisababisha vifo cha watoto pacha wenye umri wa miezi 10.
Kulingana na maelezo hayo, upande wa Jamhuri ulikuwa unadai watoto hao walikuwa wakiishi na mama yao mzazi katika chumba alichopanga na kwamba mshitakiwa alianzisha mtindo wa chuki dhidi ya watoto wake.
Kwamba mara kadhaa, aliwapiga na kuonyesha chuki, akisema alilemewa na mzigo wa kuwatunza na mara nyingi alidai waende kwa baba yao na siku ya tukio inadaiwa aliwakandamiza shingoni na kuwanyonga hadi wakawa dhaifu.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, baada ya kubaini watoto hao wachanga wamekuwa dhaifu, waliwaita majirani, akiwamo shahidi wa kwanza ambaye aliitikia wito huo na haraka aliwachukua watoto hao na kuwawahisha hospitali kwa matibabu.
Walipofikishwa hospitali, ilibainika tayari walikuwa wamefariki dunia, na hapo ndio suala hilo lilitolewa taarifa polisi na uchunguzi ukaanza mara moja na uchunguzi wa miili yao ulibaini kiini cha kifo ni kukosa hewa kulikotokana na kunyongwa.
Mshitakiwa aliyekuwa akitetewa na mawakili Roman Selasini Lamwai na Mary Masumbuko Lamwai alikanusha kusababisha vifo vya watoto pasipo kukusudia ambapo upande wa Jamhuri uliita mashahidi wanne na kutoa vielelezo viwili.
Jamhuri katika kesi hiyo waliwakilishwa na wakili wa Serikali, Grace Kibaki.
Katika hukumu yake ambayo iliwekwa katika tovuti ya mahakama Februari jana Jumanne, 10, 2026, Jaji Mtembwa alisema baada ya kupitia hati ya mashitaka, ushahidi wa Jamhuri na ule wa utetezi, swali linabaki kama shitaka dhidi yake limethibitishwa pasipo kuacha mashaka, hivyo kuiwezesha mahakama kumtia hatiani.
Jaji alisema katika kesi hiyo, hoja kadhaa hazibishaniwi na kwamba kwa kuegemea ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri namba 1, 2, 3, 4 na wa utetezi namba 1 na vielelezo, ni dhahiri Sulaiya na Suleiya ni marehemu na walikufa Septemba 28.
“Swali hapa ni je, mshitakiwa ndiye anahusika na vifo vya pacha hao?” alihoji Jaji.
Jaji alisema kifungu cha 199 cha Kanuni ya Adhabu, kinasema pale ambapo mwanamke kwa kitendo chochote cha makusudi au kuacha kutenda kitendo hicho amesababisha kifo cha mtoto wake mwenye umri wa chini ya miezi kumi na mbili.
Lakini wakati wa kitendo hicho mama alikuwa hajapona kutokana na kuzaa mtoto huyo na kwa sababu hiyo au kwa sababu inayohusiana na unyonyeshaji baada ya kuzaa mtoto huyo akili yake ilidhurika, atakuwa na hatia ya kuua bila kukusudia.
“Nikiri kwamba, hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaomhusisha mshitakiwa na vifo vya watoto wake hao wachanga ambao walikuwa na umri wa miezi 10.”
Jaji akaongeza kusema kulingana na ushahidi wa shahidi namba 1 wa Jamhuri ambaye ni mwenye nyumba, siku ya tukio saa 3:00 asubuhi, alimsikia mshitakiwa akipiga kelele akisema “Njoo uone watoto wangu hawaamki”.
Kwa kushirikiana na majirani wengine, shahidi huyo aliwachukua watoto hao na kuwawahisha hospitali na baada ya uchunguzi walibainika walikuwa wamekufa.
Shahidi wa pili ambaye ni baba mzazi wa watoto, alieleza asubuhi ya siku ya tukio, alimpigia simu mzazi mwenzake na kumuuliza ameamkaje, akiwa bado kwenye simu naye alimweleza kuwa watoto wao wako katika hali ya udhaifu.
Alisema alipata fursa ya kuzungumza na shahidi wa kwanza wa Jamhuri ambaye alimjulisha kuwa pacha hao walikuwa na tatizo la kupumua hivyo akamshauri awawahishe hospitali na akajulishwa kuwa tayari walikuwa wamefariki.
Shahidi wa 3 ambaye ni Ofisa wa Polisi, alieleza mahakama kuwa baada ya kujulishwa juu ya tukio hilo, alifika eneo la tukio na kukutana na mshitakiwa na watu wengine wakiwawahicha pacha hao hospitali na akawapa fomu namba 3.
Aliiambia mahakama kuwa alichunguza tukio hilo kwa ukaribu na alitembelea eneo la tukio na kwamba shingo za pacha hao zilikuwa na alama zikiashiria wamenyongwa na ripoti ya uchunguzi ilithibitisha hicho alichokiona.
Shahidi huyo alitoa mahakamani ripoti mbili za uchunguzi wa miili ya pacha hao (postmorterm) na maelezo ya Dk Paul Ngwa’lali kama kielelezo cha kesi hiyo.
Katika utetezi wake akiongozwa na mawakili wake, mshitakiwa alieleza mahakama kuwa siku ya tukio, alienda dukani kutoa fedha kwa njia ya kielektroniki, ambazo alikuwa ametumiwa na mzazi mwenzake na kuwaacha watoto chumbani peke yao.
Alieleza wakati aliporudi kutoka dukani, alikuta mlango upo vilevile kama alivyouacha hivyo aliingia ndani na kuendelea na shughuli zake za kwaida.
Baadaye aliamua kuwaamsha watoto wake, lakini alipowagusa, alibaini kuwa walikuwa dhaifu sana na ni katika wakati huo huo, baba mzazi wa watoto alipiga simu na akatumia fursa hiyo hiyo kumjulisha juu ya hali ya watoto anayoiona.
Alimshauri awawahishe pacha hao hospitali na kwa msaada wa majirani, waliwachukua watoto hao na kuwapeleka hospitali ya Sabina na walipofika aliambiwa akae nje, baadaye daktari alimletea taarifa kuwa wamefariki dunia.
Katika hukumu yake, Jaji Mtembwa alisema kama alivyoeleza mwanzo, katika shauri hilo kulikuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa mama wa mtoto kwa kitendo cha makusudi, alisababisha vifo vya watoto wake hao pacha.
Jaji alisema kwa kupitia kwa ukaribu ushahidi wa mama huyo, unaonyesha kuwa siku ya tukio alikwenda dukani na kuwaacha watoto peke yao chumbani, na aliporudi na kutaka kuwaasha, ndipo alipogundua wamekuwa dhaifu.
“Katika kujibu maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili wa utetezi, shahidi wa 4 ambaye alikuwa mpelelezi alikiri kutochunguza kama kweli mshitakiwa alikwenda dukani muda huo wa asubuhi kama alivyoeleza katika utetezi wake,”alisema Jaji.
“Kwa kweli, mshitakiwa anahusishwa tu kwa sababu yeye ndiye mama wa watoto wachanga waliofariki na ndiye wa mwisho kuonekana nao wakiwa hai,” alieleza.
“Kwa maoni yangu, kesi hii haikuchunguzwa vya kutosha, na kuacha masuala kadhaa bila kujibiwa,”alisema Jaji Mtembwa na kuongeza kusema kuwa;-
“Kama shahidi namba 4 angejiridhisha kama shahidi wa 2 (baba wa watoto) alikuwa amemtumia mzazi mwenzake pesa siku ya tukio na kwamba mshitakiwa alienda kuzitoa na kuwaacha watoto wenye chumbani, ushahidi wa utetezi ungekuwa umetikiswa japo kidogo,” anaeleza.
“Ushahidi uliotolewa na mshitakiwa alionyesha kuwa alipokwenda dukani kutoa pesa zilizotumwa na baba wa watoto, kuna mtu mwingine aliwanyonga watoto wake. Hili eneo halikuchunguzwa na shahidi 4 na kuacha maswali mengi.”
Jaji alisema kutokana na ukweli kuwa mshitakiwa ndiye aliwajulisha majirani akiwemo mwenye nyumba pamoja na baba wa watoto juu ya tukio lile, inaonyesha kuwa hakuwa amevurugwa na athari za kujifungua watoto hao.
“Wakati wa usikilizwaji wa kesi hii, nilichunguza ushahidi uliowasilishwa na mshitakiwa na tabia yake (demeanor) kama shahidi, nimeridhika kuwa alikuwa anasema ukweli. Kwa hivyo niliona kuwa anaaminika,”alisisitiza Jaji Mtembwa.
Jaji alisema kutokana na uchambuzi wa ushahidi na yote aliyoyaeleza, anaona kuwa makosa mawili ambayo mshitakiwa ameshitakiwa nayo hayajathibitishwa na yameacha mashaka hivyo kwa mazingira hayo anamwachia huru mshitakiwa.