Dodoma. Serikali imesema jamii ya watu wasioona ina nafasi muhimu na ya msingi katika maendeleo ya Taifa ambapo kupitia elimu, sanaa, ujuzi wa kazi mbalimbali, michezo, pamoja na mchango wao katika kuhifadhi na kuendeleza urithi wa kitamaduni, watu wasioona wameendelea kuthibitisha kuwa ni rasilimali muhimu ya Taifa.
Aidha ushirikishwaji wao kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni unaongeza tija, ubunifu na mshikamano wa kijamii, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi wa jamii na maendeleo endelevu ya Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa leo Februari 11, 2026 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na wenye Ulemavu) Ummy Nderiananga wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu maadhimisho ya siku ya breli (maandishi ya nukta nundu) yatakayofanyika kitaifa mkoani Tanga Februari 12, 2026.
Nderiananga amesema kupitia matumizi ya teknolojia ya breli na nyingine saidizi, watu wasioona wanawezeshwa kupata elimu, taarifa na maarifa yanayowawezesha kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.
Mwenyekiti wa chama Cha wasioona mkoani Dodoma, Enock Mbawa, akizungumza kuelekea katika maadhimisho ya Breli (maandishi ya nukta nundu) yatakayofanyika kitaifa Jijini Tanga Februari 12, 2026.
“Tunapoadhimisha kilele cha siku ya kimataifa ya breli duniani, ni wajibu wa jamii kwa ujumla kutafakari kwa kina juu ya nafasi na mchango wa wasioona katika maendeleo ya Taifa. Jamii inapaswa kuwatambua, kuwaheshimu na kuhakikisha wanapata haki, fursa na ushiriki sawa na wananchi wengine katika nyanja zote za maisha,” amesema Nderiananga na kuongeza kuwa,
“Maadhimisho haya yanatoa wito kwa kila mwananchi, taasisi za umma na binafsi, mashirika ya kiraia pamoja na wadau wa maendeleo kushirikiana kwa pamoja katika kuimarisha mazingira jumuishi, kuondoa vikwazo vya kijamii na kimazingira, na kuweka mifumo wezeshi itakayohakikisha ustawi na maendeleo ya jamii ya wasioona yanatimizwa kikamilifu. Kwa kufanya hivyo, Taifa letu litaendelea kujenga jamii yenye usawa, haki na mshikamano, inayothamini mchango wa kila mmoja bila ubaguzi.”
Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za makusudi katika kuhakikisha watu wenye ulemavu, hususan wasioona, wanapata haki, huduma na fursa sawa na wananchi wengine. Jitihada hizi zinalenga kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi, kisiasa na kitamaduni.
Miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na kuwepo kwa Sera ya Taifa ya Maendeleo na huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya Mwaka 2004.
Kwa upande wake, Katibu Wa Chama Cha Wasioona, Mkoa wa Dodoma, Enock Mbawa amesema ushiriki wa kundi hilo katika nyanja mbalimbali husaidia kufikisha sauti zao.
Aidha ameiomba Serikali kuwashirikisha katika programu mbalimbali lakini pia wasisahaulike katika kupata vitakavyowawezesha kufanikisha majukumu yao ya kila siku.
Kadhalika aliishauri jamii kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu kwa kuwa vifaa vya kujifunzia vipo.