MABAO mawili aliyofunga mchezaji wa Coastal Union, Bakari Msimu, katika ushindi wa timu hiyo wa 4-1, dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons kwenye Ligi Kuu Bara juzi, yamemfanya nyota huyo kuandika rekodi tatu tamu muhimu kwa kikosi hicho.
Nyota huyo alifunga mabao mawili juzi kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na mengine yakifungwa na Shiza Kichuya na Cleophace Mkandala, huku kwa upande wa bao pekee la kufutia machozi kwa maafande wa Prisons likifungwa na George Mpole.
Rekodi tamu alizoandika Msimu, ni ya kufunga bao la mapema zaidi msimu huu katika Ligi Kuu ambalo alichukua sekunde ya 58, ya pili ni ya kufunga mabao yake ya kwanza, huku ya tatu ni ya kuifungia timu hiyo bao la kwanza ugenini msimu huu.
Tangu msimu umeanza, bao hilo la sekunde ya 58, ndilo la mapema zaidi kufungwa na kuwa rekodi mpya, ikisubiriwa kuona atakayeivunja huko mbele, huku pia mabao yake hayo mawili ni ya kwanza kwake akiwa na kikosi hicho.
Pia, bao hilo la kwanza alilolifunga ni la kwanza kwa kikosi hicho ugenini katika mechi za Ligi Kuu Bara kwa msimu huu, kwa sababu kabla ya hapo timu hiyo ya ‘Wagosi wa Kaya’, ilikuwa haijawahi kufunga zaidi ya kuambulia suluhu au kichapo.
Mechi na Prisons ilikuwa ni ya saba kwa Coastal Union kucheza ugenini msimu huu, ambapo sita zilizopita kabla ya hiyo iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa, huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikiwa haijafunga bao lolote lile.
Kwa maana hiyo, mechi dhidi ya maafande wa Prisons imeifanya Coastal Union kupata bao lake la kwanza ugenini msimu huu, huku kwa sasa kikosi hicho katika mechi saba kati ya 14, imefunga mabao manne na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 10.
Ushindi huo kwa Coastal Union, ni wa pili kwa kocha, Mohamed Muya, tangu ajiunge rasmi na kikosi hicho, Oktoba 6, 2025, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Alli Mohammed Ameir, aliyeondoka rasmi Oktoba 1, 2025, kutokana na matokeo mabaya.
Tangu Oktoba 6, 2025, Muya aliyezifundisha timu mbalimbali zikiwamo za Fountain Gate na Geita Gold, ameiongoza Coastal Union katika mechi 11 za Ligi Kuu Bara, ambazo kati ya hizo ameshinda mbili tu, sare tano na kuchapwa nne.